Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo taasisi za kifedha, ili kuwekeza katika tafiti na bunifu zinazofanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu na wahitimu, kwa lengo la kupata suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii.
Akizungumza leo Mei 5, 2026 Dar es salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati wa uzinduzi wa shindano la iMbeju-UDSM Startup Challenge, amesema serikali inaona umuhimu mkubwa wa kuibua na kuendeleza mawazo ya ubunifu kutoka kwa vijana ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema shindano hilo linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), linalenga kuwawezesha wanafunzi na wahitimu wenye bunifu na tafiti zenye tija, huku likitoa fursa ya kupata ufadhili na mafunzo ya kitaalamu.
CRDB Foundation imeingia ubia na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kusaidia kukuza bunifu na tafiti za wanafunzi pamoja na wahitimu wa chuo hicho, ili ziweze kufikia hatua ya kuingia sokoni.
Profesa Mkenda amewasisitiza wanafunzi kutumia fursa hiyo kwa uzalendo na uadilifu, akibainisha kuwa changamoto ya ukosefu wa ajira inaweza kupungua ikiwa vijana watatumia ubunifu wao kuanzisha miradi yenye tija.
“Fedha mara nyingi huonekana kuwa changamoto, lakini kupitia juhudi za taasisi kama CRDB, sasa fursa za mitaji zinapatikana. Kilichobaki ni vijana kutumia akili zao vizuri na kuja na ubunifu unaoweza kutatua matatizo halisi ya jamii,” amesema.
Ameongeza kuwa bunifu nyingi alizoziona katika maonyesho hayo zimemvutia, ikiwemo maabara inayotembea inayoweza kusaidia shule zisizo na vifaa vya kutosha, pamoja na trekta la kilimo lililobuniwa na kijana aliyefikia elimu ya kidato cha nne.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema dirisha la kutuma maombi ya kushiriki katika programu hiyo limefunguliwa rasmi kuanzia Mei 5, 2026 hadi Juni 4, 2026.
Amesema kupitia ushirikiano huo, wanatarajia kuwawezesha vijana 100 waliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na wahitimu wake, kwa kuwapatia mafunzo na kuwasaidia kuendeleza mawazo yao ya kibunifu hadi kufikia hatua ya kibiashara.
“Tumeona kuna vijana wengi wenye ubunifu mkubwa ambao wameweza kujiajiri baada ya kupitia UDSM. Kupitia ubia huu, tutawasaidia kuboresha mawazo yao na kuyawezesha kuingia sokoni,” amesema Mwambapa.
Aidha, amewahimiza wanafunzi na wahitimu wote kuwasilisha maombi yao kupitia mifumo rasmi ya mtandaoni ili kupata fursa ya kushiriki, ambapo watakaofanikiwa watapatiwa mafunzo maalum kupitia kambi za ubunifu zitakazoendeshwa na wataalam mbalimbali.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, ameishukuru CRDB Foundation kwa kuingia ubia huo, akieleza kuwa utasaidia kukuza vipaji vya wabunifu na watafiti, na kutoa fursa kwa vijana wasio na mitaji kuendeleza bunifu zao.
Amesema shindano la iMbeju-UDSM Startup Challenge linatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko kwa vijana wengi, kwa kuwapa nafasi ya kubadili mawazo yao kuwa miradi halisi yenye tija kwa jamii.






