JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 53 wanaodaiwa kuhusika na makosa mbalimbali katika kipindi cha kuanzia Aprili 1, 2026 kufuatia operesheni endelevu za kuimarisha ulinzi na usalama mkoani humo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi wakati akizungumza na wanahabari alisema kuwa miongoni mwa waliokamatwa ni Ramadhani Mussa (33), dereva mkazi wa Dar es Salaam, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kutoa taarifa za uongo kuwa aliibiwa sehemu za siri.

Wengine ni Mussa Kaundi (39), mfanyabiashara wa Mafinga, pamoja na watuhumiwa wawili mmoja mkazi wa Isakalilo ndani ya Manispaa ya Iringa na mwingine wa Usokami, Mafinga ambao wanadaiwa kutoa taarifa za uongo kuhusu kuibiwa sehemu za siri. Uchunguzi wa kitabibu ulithibitisha kuwa taarifa hizo hazikuwa za kweli, na upelelezi umekamilika tayari kwa wao kufikishwa mahakamani.

Katika taarifa hiyo, jeshi la polisi lilieleza kuwa watuhumiwa wengine sita wamehukumiwa vifungo vya miezi mitatu hadi miaka mitatu kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo kujeruhi, wizi, shambulio, kutishia kuua na uvunjaji. Miongoni mwao ni Ernest Simagwa (44) aliyehukumiwa miaka mitatu jela kwa kujeruhi, na Baraka Nyamba (20) aliyepewa kifungo cha miezi sita kwa kosa la uvunjaji.

Kupitia operesheni hizo, polisi pia wamekamata mali mbalimbali zinazohusishwa na wizi, zikiwemo pikipiki tano, sabufa saba, runinga tano, bajaji moja aina ya TVS, kompyuta aina ya Dell pamoja na microwave moja.