Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kongowe
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, Mwajuma Nyamka, amesisitiza Serikali za mitaa pamoja na viongozi wa chama hicho kuimarisha mahusiano katika maeneo yao ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu.
Amesema baadhi ya maeneo yamekuwa yakijisahau kuwa CCM ndiyo msimamizi wa utekelezaji wa Ilani ya chama, jambo linalochangia kudhoofisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika muendelezo wa ziara yake katika Kata ya Kongowe, yenye lengo la kushukuru wananchi na wanachama wa CCM kwa kukiunga mkono chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Nyamka alisema haikubaliki kwa mitaa kukaa na fedha za miradi hadi zinarejeshwa wakati chama kipo.
“Endapo mitaa inakaa na fedha hadi zinarejeshwa, maana yake CCM imeshindwa kusimamia,” alisema Nyamka.
Kutokana na hali hiyo, aliielekeza CCM Kata ya Kongowe kusimamia kikamilifu jukumu hilo kwa kuhamasisha mahusiano mazuri kati ya Serikali za mitaa, matawi ya CCM pamoja na kuwashirikisha mabalozi katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha, akizungumzia changamoto ya baadhi ya wakazi kufunga barabara za ndani zinazoelekea kwenye makazi yao, hali inayosababisha ugumu wa kufikika kwa huduma za dharura kama zimamoto au wagonjwa, Nyamka alitoa maagizo ya kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.
Alimuelekeza Mwenyekiti wa kata, kwa kushirikiana na viongozi wengine wa kata pamoja na Diwani, kumuita Ofisa Mipango Miji na Mazingira ili kukagua maeneo yenye malalamiko na kuchukua hatua stahiki.
“Kero hii isimamiwe kwa ukaribu, na baada ya wiki moja nitarudi kuona utekelezaji wake, Viongozi tunapaswa kushuka chini kujionea changamoto kama hizi badala ya kubaki maofisini,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kongowe, Saimon Mbelwa, alipokea maelekezo hayo na kueleza kuwa kamati ya siasa ya kata, halmashauri, mkutano mkuu pamoja na viongozi wa matawi watasimamia kikamilifu utekelezaji wake.
Aliongeza kuwa walifanya ziara za chama katika kata hiyo zilizolenga kurejesha imani kwa mabalozi na wanachama, na kuimarisha shughuli za chama ikiwemo kuongeza kasi ya upandishaji wa bendera.
Naye mkazi wa Kongowe, Munira Abdallah, alieleza changamoto ya ubovu wa barabara kuelekea Forest, akikiomba chama kisimamie tatizo hilo kwani barabara hiyo ina mashimo, madimbwi na haina mifereji.
Akijibu hoja hiyo, Diwani wa Kata ya Kongowe, Hamis Shomari alieleza, barabara hiyo ipo katika hatua za utekelezaji, ambapo Serikali tayari imeshatoa fedha kwa kipande cha awali na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza kazi ya uwekaji lami na ujenzi unaendelea kwa awamu hadi Bagamoyo.







