Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi imelipongeza Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa kuboresha Kiwanda cha KMTC na kuendelea na uzalishaji wa vipuri pamoja na mashine mbalimbali kama ilivyokusudiwa wakati wa uanzishaji wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kupitia kitengo cha mawasiliano na masoko NDC,Machi 13 ,2024 ,pongezi hizo zimetolewa na mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Mjini Deo Mwanyika mara baada ya kamati hiyo ya kudumu ya Bunge kutembelea kiwandani hapo na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika katika kiwanda hicho kilichopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Aidha Mwanyika amesema kuwa KMTC ni kiwanda kikubwa cha kuzalisha viwanda vingine na kina mchango mkubwa kwenye uchumi huku akibainisha kuwa malighafi kubwa ya kiwanda hicho ni chuma kinachotumika kutengeneza vipuri na mashine na kama Taifa tukitaka kufikia malengo lazima tuanze Uchimbaji wa chuma cha Liganga.

“Nimshukuru Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kiwanda hiki kwenye matumizi ya chuma, hivyo kuamua kutoa fedha za fidia kule Liganga ili chuma kile kitumike kiwandani hapa,” amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji ameeleza kuwa wao kama Wizara yenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya viwanda hapa nchini wanafurahi kuona kazi ya kuyeyusha chuma imeanza kiwandani hapo hivyo kurejesha ajira kwa Watanzania ambao walikosa ajira kwa muda mrefu, huku akiishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizofanikisha ujenzi wa tanuru la kuyeyusha chuma (foundry) Pamoja na mtambo wa kutia utandu kwenye chuma (Galvanising plant).

“Ninamshukuru sana Mh. Rais wetu kwa maono yake na kuyatekeleza maono hayo na amewathibitishia Watanzania kuwa Taifa letu litajengwa kwa Uchumi wa viwanda hasa viwanda mama kama KMTC,” amesema Dkt. Kijaji.

Hata hivyo akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mh. Amir Mkalipa amewakaribisha wafanyabiashara mbalimbali kununua bidhaa zinazozalishwa na KMTC pia amewataka wenye viwanda kutohangaika kutafuta vipuri vya mitambo yao na kulazimika wakati mwingine kuagiza nje ya nchi kwani KMTC wana uwezo wa kuchonga vipuri hivyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe ameeleza kuwa bidhaa zinazozalishwa na KMTC zinagusa sekta mbalimbali kama kilimo, viwanda, uchukuzi, usafirishaji, madini, misitu na ujenzi hivyo kuwa ni kiwanda chenye manufaa katika sekta hizo.

Licha ya kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa jitihada inazozifanya katika kukiendeleza kiwanda hicho Dkt. Shombe amebainisha kuwa Serikali imeendelea kufanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha kiwanda hiki kinaboreshwa na hatimaye kiweze kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda nchini na kuinua maisha ya wananchi na kutoa ajira ambapo mpaka hivi sasa ujenzi wa tanuru la kuyeyusha chuma pamoja na mtambo wa kutia utandu kwenye chuma umeshakamilika.

By Jamhuri