Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi – Dar es Salaam

Kituo cha Utafiti cha Jeshi la Polisi kilichopo Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam kwa kushirikina na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) imeendelea na mafunzo awamu ya pili kwa kundi la wanafunzi wa kozi ya uofisa ambayo yamelenga kuwajengea uwezo na maarifa mapya katika kupambana na ukatili wa kijinsia.

Akiongea leo Agosti 07,2023 Mkuu wa kitengo cha utatifi cha Jeshi la Polisi kilichopo chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA) kamishna msaidizi wa Polisi ACP Ralph Meela amesema kuwa kazi kubwa ya kituo hicho ni kufanya tafiti na kushirikiana na Taasisi za Elimu ya Juu katika kuwaongezea uwezo maafisa maafisa na askari wa Jeshi hilo.

Ameongeza kuwa tayari zaidi ya yaasisi kumi zimeshafika chuoni hapo kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa maafisa wanafunzi na wakaguzi wasaidizi wa Polisi huku akimshuru Mkuu wa Jeshi hilo IGP Camillus Wambura kwa namna ambavyo amewaunganisha na yaasisi za elimu ya juu katika kufanya maboresha ya utendaji kazi unaoendana na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia.

Kwa upande wake mhadhiri msadizi kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru Elinami Nassari amebainisha kuwa ni muhimu Jeshi la Polisi kushirikisha Jamii na kuzielewa kwa kina Jamii ambazo wanakwenda kuzihudumia ambapo amewaomba maafisa hao wanafunzi kufahamu mila na tamaduni husika ili kutengeneza ushirikishwaji wa Jamii kikamilifu na wenye matokeo chanya.

Nae Mwanafunzi wa kozi ya Uofisa Rose Mbaga amesema Mafunzo hayo kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru yamewaongezea uwezo na maarifa mapya katika mapambano dhidi ya ukatili ya kijinsia.

Sambamba na hilo mwanafunzi wa kozi ya Uofisa Issa Asali amewaomba wanafunzi wenzake mara watakapo maliza mafunzo yao ya Uofisa na kupangiwa kazi na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Kwenda kutumia njia rafiki walizofundishwa na wahadhiri Pamoja na wawezeshaji kutoka Taasisi ya maendeleo ya Jamii Tengeru.

By Jamhuri