Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani 

Kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo ,mkoani Pwani kimeshuka kutoka asilimia 5.9 hadi kufikia asilimia 5.5.

Akitoa hali ya kiwango Cha maambuzi ya ugonjwa huo, katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani Mkoani Pwani yaliyofanyika viwanja vya shule ya msingi Mtongani, Kibaha ,mwakilishi wa mkuu wa mkoa huo ,Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri, ameeleza kiwango hicho kimeshuka kati ya kipindi cha mwaka 2012 hadi 2017.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri akiwa kwenye

Alieleza ,mbali ya mafanikio hayo Halmashauri ya Kibaha Mjini , Mkuranga na Chalinze bado zina maambukizi makubwa kutokana na changamoto ya muingiliano wa idadi ya watu wanaotoka nje ya halmashauri hizo.

Aidha ,Sara ameeleza kundi la vijana pamoja na wanaume wanaonekana kuwa na mwamko mdogo wa kujitokeza kupima afya zao.

Alifafanua , katika kipindi cha mwezi January Hadi Novemba mwaka huu takwimu zinaonyesha ,kuna maambukizi mapya ya vijana 1,004 wenye umri kati ya miaka 15-24 .

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali kwenye maadhimishi ya Siku ya Ukimwi Duniani mkoani Pwani

“Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni IMARISHA USAWA, Lazima tuweke usawa ,unaweza kuona vijana hawa ni wadogo ,Lakini tukumbuke umri huu ni wa kukua ,na ndio wanaojiingiza katika maadili yasiyo mema ikiwemo madada poa,wavuta bangi na madawa ya kulevya hivyo kujikuta wakipata maambukizi ya virusi hivyo”alisema Sara.

Alieleza,hali ya kutojua hali zao za maambukizi ya vvu huleta athari kubwa kwa familia zao na inadhoofisha mapambano kwa mkoa na zaidi kushindwa kufikia malengo ya Millennia ya kupambaba na ukimwi ya mwaka 2020 na 2030″alisisitiza Sara.

Awali muathirika wa VVU kutoka kata ya Kikongo, Elizabeth Ngonyani ameeleza ,kuugua Ukimwi sio kufa kwani tangu agundulike kuwa na ugonjwa huo ,na wapo waliokufa na kumuacha yeye akiwa afya njema.

Aliishukuru Serikali pamoja na THPS kwa kutoa huduma bora na Dawa kwa WAVIU.

Nae Dkt.Sisty Moshi kutoka THPS alieleza ,THPS inafadhiliwa na Serikali ya Marekani na inashirikiana na mkoa huo kwa miaka kumi Sasa .

Amesema kiwango Cha upimaji mkoa upo kiwango Cha asilimia 95 na walio kwenye dawa za kufubaza VVU ni takriban watu 50,000 sawa na asilimia 98.

Moshi alieleza, kwa mwaka huu wametoa fedha Bilioni 3.2 kwa ajili ya shughuli za Halmashauri.

Kaimu Katibu Tawala mkoani Pwani,Rukia Mhango aliishukuru THPS ,AMREF na wadau wengine wa jamii kwa kuboresha Mazingira ya utoaji huduma za kiafya .

Amewaasa ambao wamegundulika na VVU na kuanza dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi wasiache dawa na wasiwe watoro kufuata dawa na kuhudhuria kliniki zao.