Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imeanzisha kliniki ya matibabu ya moyo inayoanza saa kumi jioni hadi saa mbili usiku ili kutoa nafasi kwa wagonjwa walioshindwa kufika kliniki za asubini kupata huduma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amesema kuanzishwa kwa kliniki hiyo kumelenga kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo.

Dkt. Kisenge amesema kuna wagonjwa ambao wanashughuli nyingi wakati wa asubuhi na pia baadhi ya wazee wanashindwa kuamka alfajiri kwa ajili ya kuwahi kliniki lakini kuwepo kwa kliniki ya jioni kutawasaidia wagonjwa wote kupata muda wa kuhudhuria kliniki zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo kuhusu Kliniki mpya ya matibabu ya moyo inayoanza saa kumi jioni hadi saa mbili usiku aliyoizundua jana jijini Dar es Salaam.

“Tumeanzisha kliniki mpya ya matibabu ya moyo ambayo itakuwa inaanza saa kumi hadi saa mbili usiku lengo likiwa ni kuwasaidia wagonjwa ambao wanataka kupata huduma za matibabu ya moyo wakati wa jioni.

“Taasisi yetu imekuwa ikipata wagonjwa takribani 400 kila siku na wengine wengi wanahitaji kupata huduma za matibabu lakini hawapati kwasababu wanakosa muda na nafasi ya kutibiwa katika siku husika, hivyo basi tumeona tuendelee kuimarisha huduma na kuwasaidia hasa wazee ambao wanashindwa kuamka asubuhi na kuwahi kliniki,” amesema Dkt.Kisenge.

Dkt. Kisenge amesema kuwepo kwa kliniki ya jioni kutatoa fursa kwa wagonjwa wa moyo ambao wanafanya kazi za kuajiriwa kwani watapata nafasi ya kwenda kazini na baada ya majukumu yao ya kazi watafika katika taasisi hiyo kwa ajili ya kupatiwa huduma katika kliniki ya jioni.

“Tunaendelea kuboresha huduma zetu na sasa tutakuwa tunawafuata wananchi mahali walipo ambapo tumejipanga kuzunguka zaidi ya mikoa 15 ili tuweze kuwapatia huduma za matibabu ya moyo na kutoa elimu kwa madaktari walioko mikoani ili na wao waweze kuwabaini na kuwapatia huduma wagonjwa wetu moyo”, alisema Dkt. Kisenge.

Akizungumzia kuhusu kliniki hiyo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo aliyebobea katika kutoa huduma za vipimo vya moyo Henry Mayala alisema kliniki hiyo ya jioni itatoa fursa pia kwa wagonjwa hao kufanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo.

“Siku za nyuma vipimo vya magonjwa ya moyo vilikuwa vinatolewa kwa idadi na wagonjwa wengine kupewa tarehe za kurudi kwa ajili ya vipimo husika lakini kupitia kliniki hii ya matibabu ya moyo inayoanza jioni tutaendelea kutoa huduma za vipimo kwa wagonjwa wengi zaidi,”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpima shinikizo la damu na kiwango cha oksijeni kwenye damu mgonjwa aliyehudhuria kliniki mpya ya matibabu ya moyo inayoanza saa kumi jioni hadi saa mbili usiku wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

“Kupitia kliniki ya jioni iliyoanzishwa tutaenda kupunguza msongamano wa wagonjwa wetu kwani vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography-ECHO) na vipimo vya kuangalia mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography-ECG) vitakuwepo kuanzia asubuhi hadi saa mbili usiku,” amesema Dkt. Mayala.

Kwa upande wa wagonjwa waliohudhuria kliniki hiyo walishukuru kwa kuanzishwa kwa huduma ya kliniki ya jioni ambayo inatoa nafasi kwa wagonjwa wengi zaidi kupata nafasi ya kutibiwa.

“Ninaushukuru uongozi wa JKCI kwa kuanzisha kliniki ya jioni kwani kwa kupitia kliniki hii kutarahisisha upatikanaji wa matibabu hasa kwa watu wazima ambao kuamka asubuhi ni changamoto,”.

“Hapo awali ilitulazimu kufika JKCI alfajiri lakini kutokana na idadi ya wagonjwa kuwa wengi tulijikuta tunakaa hadi jioni lakini kupitia kliniki hii ya jioni tutakuwa tunakuja mchana kupata huduma bila msongamano na kurejea nyumbani kwa wakati,” amesema Omary Chudi.

Halima Mbaga anayetibiwa katika Taasisi hiyo amesema kliniki ya jioni ya matibabu ya moyo inawapa fursa wagonjwa wa moyo kufika JKCI wakati wowote kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu na vipimo vya magonjwa ya moyo.

By Jamhuri