Na Mathias Canal, JamhuriMedia,Simiyu

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Livingstone Lusinde ameitaka serikali kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na Watanzania wenye nia njema kuhusu sakala la bandari ya Dar es Salaam na kuyafanyia kazi.

Lusinde amebainisha hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa baraza kuu la jumuiya ya wazazi ya Chama Cha Mapinduzi-CCM Wilaya ya Bariadi lilifanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Alliance leo tarehe 14 Julai 2023.

Amesema kuwa maoni hayo yanatosha ni wakati sasa wa serikali kuyafanyia kazi badala yake iachane na mambo mengine ikiwemo kutoa elimu.

“Maoni yametolewa mengi ya viongozi wa dini, ya wanasheria, ya wasomi, serikali iyachukue na kuendelea kufanya kazi ilizojipangia” Amesisitiza Lusinde na kuongeza kuwa

“Hivi kama kwenye mpira wa mguu kusingekuwa na refa wa kuamua magoli mpira ungechezwaje, yaani kungekuwa na watu ukifunga goli waanze kujadiliana lile goli ama sio goli”

Amesema serikali imeshasikia maoni yachujwe na yenye nia njema yafanyiwe kazi na kufunga ajenda hiyo ili kuendelee na kazi.

Naye Mbunge wa Vitimaalum Zanzibar Mhe Tauhida Cassian Galoss amewataka Watanzania kuhakikisha kuwa hawakubali wala Kuthubutu Kukubali Kutikiswa kwa Muungano wa Tanzania.

“Watanzania kutoka Kigoma mpaka Zanzibar ni wamoja hivyo hawapaswi kugombanishwa wala kutenganishwa na mtu yeyote” Amesisitiza Mhe Tauhida

Amesema kuwa umoja na mshikamano wa Tanzania unasababisha watu wengine kuona wivu na choyo.

Akizungumza katika mkutano huo Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mkoani Simiyu Mhe KUNDO MATHEW amewataka Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi-CCM kuwa Mabalozi Wazuri wa Maendeleo Yanayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan.


Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo mgeni rasmi- Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Mhe Livingstone Lusinde (Mb).

By Jamhuri