Na Mwandishi Wetu,Jamhurimedia,Morogoro

MAMLAKA ya udhibiti usafiri ardhini( LATRA)imesema kuwa kuanzia Septemba mosi 2022 mabasi yote ya abiria ambayo hayatakuwa yamewakatia abiria wake tiketi mtandao hayataruhusiwa kuendelea na safari yake ikiwa ni pamoja na kutozwa faini ya shilingi 250000 kwa atakayekiri kosa.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ukaguzi wa tiketi mtandao kwa mabasi ya abiria yanayoenda mikoani na nchi jirani katika kituo cha mabasi cha Msamvu Mkoani Morogoro uliyofanywa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha cha usalama barabarani kaimu mkuu kitengo cha mawasiliano wa LATRA Salum Pazzy alisema kuwa zoezi hilo la ukaguzi ni endelevu mpaka pale wasafirishaji wote watakapotumia tiketi mtandao.

Aidha amesema kuwa msafirishaji atakayebainika kutoa tiketi za mkono na kukiri kosa atatozwa faini ya shilingi 250000 ambapo alisema kuwa kwa ambao hawatakiri makosa watalazimika kuwapeleka mahakamani ambapo faini yake ni shilingi 500000 au jela miezi sita au vyote viwili kwa pamoja.

Hata hivyo alisema kuwa katika ukaguzi wao wamebaini kuwa baadhi ya mabasi ya mikoani pamoja na yanayoenda nchi jirani bado hayajaanza kutoa teketi mtandao na hivyo kuwataka wamiliki kuhakikisha wanatoa tiketi kwa njia ya mtandao vinginevyo hawataruhusiwa kuendelea na safari.

Aidha alisema wasafirishaji hao wanapaswa kutambua kuwa tiketi mtandao zinapaswa kutolewa kwa abiria wote kuanzia mwanzo wa safari pamoja na wanaopandia njiani ambapo alisema kuwa baadhi ya wasafirishaji hawataoi tiketi mtandao kwa abiria wanaopandia njiani kwa kisingizio cha mtandao.

“hivi kweli mtu anapandia gari chalinze unashindwaje kumkatia tiketi mtandao kwa kisingizio cha kusumbuliwa na mtandao hicho kitu hakikubaliki,maana karibu eneo kubwa lina miji na mtandao upo wa kutosha”alisema

Hivyo aliwataka kuacha visingizio wanapaswa kukata tiketo hizo kwa mujibu wa sheria ambapo alisema kuwa walishawaongezea muda mara kadhaa na unatosha hivyo ni wajibu wao kutii sheria bila shuruti ambapo alisema kuwa msafirishaji atakayebainika kutoa tiketi za mkono atatozwa faini hizo ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani.

Akizungumza kwa niaba ya abiria wenzake Salama Ramadhani aliishukuru Serikali kwa kuendesha zoezi hilo ambapo alisema kuwa awali walikuwa wanapata changamoto ambapo gari ikipata hitilafu walikuwa wanakosa msaada kutoka kwa wasafirishaji na kwamba kwa kupitia tiketi mtandao LATRA wapo wanaweza wakatoa msaada pindi wanapopata matatizo.

Naye mmoja wa madalali wa kukatisha tiketi katika kituo hicho cha mabasi maarufu kama ‘sarange’ Fikiri Jumanne alisema kuwa zoezi hilo linaonekana kuathili sana wao ambao ni kundi la vijana ambao wamejiajiri kwa kuwapeleka abiria kwenye mabasi na kupatiwa fedha kidogo za kujikimu ambapo kwa sasa itakuwa changamoto kwao kutokana na kuwa fedha zote zitaingia kwenye mfumo na wao kuambulia patupu.

Hata hivo aliwaomba wasafirishaji na wamiliki kuona namna ya kuongeza fedha kwenye tiketi mtandao ili nao waweze kupata fedha za kujikimu kupitia kazi yao hiyo.

Ukaguzi huo wa tiketi mtandao umefanywa kwa mabasi ya abiria 78 yaliyoingia na kutoka katika kituo hicho ambapo umebaini kuwa asilimia 98 ya wasafirishaji wameshaanza kutumia tiketi Mtandao na kwamba asilimia 2 tu ndio bado hawajaanza kutumia tiketi hizo yakiwemo mabasi yanayoenda nchi jirani.

By Jamhuri