Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla ametoa mwezi mmoja kwa wavamizi wa ardhi ya Kiwanda Cha Wazo kuhakikisha wanapokea ankara na kuanza malipo ya fidia kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwa yamewekwa awali.

RC Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa kupokea taarifa ya mwenendo wa zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wa Chasimba, Chatembo na Chachui ambapo amesema endapo wananchi watakaidi agizo hilo Serikali itajitoa rasmi katika kuwadhamini na kuachia kiwanda kutekeleza amri ya mahakama ambayo ni bomoabomoa.

Aidha RC Makalla amesema taarifa inaonyesha kati ya wavamizi wote 4,070 ni wavamizi 39 pekee sawa na asilimia 9 wamelipa na wanastahili hati, 150 wamelipa ada ya kuomba kupata hati na 3,881 wamekaidi kulipa.

Kuhusu wavamizi wapya waliovamia upya eneo la kiwanda na eneo la Jeshi la Wananchi, RC Makalla amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuhakikisha wavamizi hao wanaondolewa mara moja.

Pamoja na hayo RC Makalla amewahimiza wavamizi hao kujiadhari na wanasiasa wanaotumia zoezi hilo kama mtaji wa kisiasa kwa kuwa jambo hilo limekaa kisheria.

Itakumbukwa kuwa zaidi ya wananchi 4,070 walivamia eneo la Kiwanda Cha Wazo ambacho ni mmiliki halali wa eneo hilo na Mahakama ilitoa amri ya kuondoshwa kwa wananchi hao baada ya kushindwa kesi jambo lilowalazimu kuiangukia Serikali iwasaidie kutafuta muafaka na baada ya mazungumzo baina ya Serikali na Kiwanda iliamuriwa walipe kiasi cha Shilingi 6,419 kwa Mita za mraba badala ya 40,000 iliyopendekezwa na kiwanda lakini Cha kushangaza Wwnanchi hao wamekaidi kulipa fidia hiyo.

By Jamhuri