Mbilia Bel astaafu muziki

NA MOSHY KIYUNGI
Tabora

Mwimbaji mkongwe wa muziki wa Kilingala na Kifaransa, Mbilia Bel, amestaafu rasmi muziki Januari mwaka jana.
Mwana mama huyo mapema Januari 2017, alitangaza kustaafu kwake wakati akisherehekea miaka 40 kwenye muziki, pia siku yake ya kuzaliwa kwa kutimiza miaka 58.

Mbilia mwenye umri wa miaka 59, alianza kujiingiza kwenye kazi ya muziki akiwa na umri wa mika 17, akiwa msichana mdogo ambapo hadi sasa ametimiza miaka 40 tangu aanze kazi ya uimbaji.
Mwanamuziki huyo alisema kuwa ameachia albamu yake mpya ya mwisho inayoitwa ‘Signature’, inayohusu maisha yake yanayoangazia uzuri wake na ubaya.
Amesema kwamba baada ya kuachana na kazi hiyo ya uimbaji, ataendelea kuwa mshauri wa wasichana chipukizi wanaowania kuingia katika tasnia ya muziki hivi sasa.

Mwana mama huyo mashuhuri, yasemekana kuwa kustaafu kwake kutoka kwenye tasnia ya muziki kulikuja mwezi mmoja baada ya kuzuka kwa taarifa kwamba amefariki dunia.
Alipata sifa kubwa katika miaka ya 1970 na 1980 kutokana na sauti yake nyororo. Umaarufu wake ulipatikana baada ya kujiunga na mwanamuziki, Tabu Ley Rochereau, ambaye alikuwa akitunga naye nyimbo na kuziimba kwa umahiri mkubwa.
Kwa mfano, wimbo wake wa ‘Eswi Yo Wapi’, unaomaanisha ‘Kwa Nini Umekerwa?’, ukiwa ni wimbo wa fumbo baada ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Rochereau.
Bel aliingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na Tabu Ley na hatimaye walifunga ndoa ya kifahari ambayo ilifanyika ndani ya ndege.

Katika kipindi cha ndoa yao, Mbilia Bel na Tabu Ley walifanikiwa kupata mtoto wa kike, Meledoy Tabu, ambaye pia ni mwanamuziki hivi sasa.
Pamoja na kustaafu kwake, lakini katika ukanda wa Afrika Mashariki, Mbilia Bel, ataendelea kukumbukwa hasa kutokana na wimbo wake wa ‘Nairobi’.

Wasifu wake

Majina yake halisi anaitwa Marie Claire Mbilia Mboyo (Mbilia Bel), alizaliwa mwaka 1959 jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mwaka 1977, akiwa na umri wa miaka 17 aliacha shule na kujiunga na kundi la mwanamke muimbaji maarufu wakati huo, Abeti Masikini, akiwa mcheza ‘show’.
Baada ya miaka minne katika kundi hilo alijiunga na mwanamuziki, Sam Mangwana, katika maonyesho mbalimbali nchini Kongo. Mwishoni mwa mwaka 1981 aliweza kufanyiwa usaili na Tabu Ley na siku hiyohiyo kuajiriwa katika kundi la Afrisa International na ndipo alipopewa jina la Mbilia Bel.
Alikuwa mzuri wa sura, umbo na sauti yake ya juu ‘soprano’, iliwezesha kundi la Afrisa kuanza kupata umaarufu mpya.
Wimbo wake wa kwanza ‘Mpeye Ya Longo’ ambao tafsiri yake ni ‘Roho Mtakatifu’ uliorekodiwa mwaka 1982 ulikuwa ukieleza kuhusu shida anazopata mwanamke aliyeachwa katika ndoa na ulipendwa sana na wanawake wa Kongo wakati huo.
Wimbo huo uliotungwa na Tabu Ley ulipendwa zaidi, ulikuwa unaelezea matatizo ya mwanamke na ulikuwa unaimbwa na mwanamke.

Hatimaye wimbo huo ulishinda tuzo ya wimbo bora nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (zamani Zaire) mwaka 1983, pia Mbilia akashinda tuzo ya msanii mpya bora.
Katika kipindi hicho tasnia ya muziki wa Kongo ilikuwa ikitawaliwa na wanaume watupu, kwa hiyo wimbo huo ulikuwa ufunguo kwa waimbaji wa kike wa Kongo na hatimaye hata waimbaji wa kike hapa kwetu Tanzania.
Wimbo mwingine maarufu sana nchini ni ‘Yamba Ngaa’, unaomaanisha ‘Nipokee Mpenzi.’ Ulitungwa na Tabu Ley na kuimbwa na Mbilia Bel kwa sauti nyororo.

Kibao kilichofuata kilikuwa ni ‘Eswi Yo Wapi’ (Uliumizwa Wapi?), huu ulikuwa wimbo ambao Mbilia na Tabu Ley walitunga kwa pamoja nao ukawa maarufu sana.
Kutokana na kuwepo kwa Mbilia, umaarufu wa Afrisa uliendelea kukua na kuanza kuvunja ngome kongwe ya TP OK Jazz katika mauzo na umaarufu.
Maonyesho ya bendi ya Afrisa yalijaza sana na kivutio kikubwa kilikuwa Mbilia ambaye alikuwa anajua kulitawala jukwaa na mara nyingi alijiunga na wanenguaji wa Afrisa walioitwa Rocherreautes kutokana na jina la Tabu Ley Rochereau.
Kwa pamoja walikuwa wakicheza vizuri, kazi ambayo ndiyo aliyoanzia katika ulimwengu wa muziki.

Kama kawaida, umaarufu una matatizo yake, kufikia mwaka 1986 uhusiano kati ya Tabu Ley na Mbilia ukaanza kuingia nyongo, ukaibuka uvumi kuwa Mbilia alitaka kujitoa maisha baada ya onyesho kubwa sana Kinshasa lilioitwa Music-Media ‘86.’
Utata ukazidi  baada ya Tabu Ley alipoongeza idadi ya wanawake katika bendi yake, hasa ujio wa Kishila Ngoyi, ambaye alipewa jina la kisanii la Faya Tess.
Pamoja na minong’ono hiyo, wasanii wote wawili walikataa katakata kuwa kulikuwa na tatizo baina yao.

Baada ya kuingia kwa Faya Tess, Afrisa ilifanya safari ya maonyesho Afrika Mashariki ambayo matokeo yake ndiyo nyimbo kama ‘Nadina’, ambapo wimbo huo uliimbwa kwa Kiswahili na Kilingala.
Hatimaye Mbilia Bel aliiacha Afrisa mwishoni mwa mwaka 1987 na kuwa mwanamuziki wa kujitegemea.

Baada ya kuvunjika kwa uhusiano wake na Tabu Ley, Mbilia Bel aliunda bendi yake mwenyewe na kuimba nyimbo nyingi kama ‘Manzili Manzili’ kwa lugha yao ya Kinyansi, kutoka Jimbo la Bandundu, kusini magharibi mwa DRC.
Baadaye alielekea Paris, Ufaransa alikojiunga na mpiga gitaa, Rigo Starr Bamundele.

Huko alitengeneza albamu yake ya kwanza iliyoitwa ‘Phénomène’, ambayo ilipata umaarufu mkubwa nchini DRC na hata nje ya Kongo. Lakini kazi zake zilizofuata hazikufikia umaarufu ule na kwenye bendi aliyoihama ya Afrisa, pia kukawa na matatizo kwani Tabu Ley naye alionekana kuishiwa ari ya kutunga vibao vipya na kusababisha kuwa mwisho wa Afrisa International.
Mbilia Bel alikwenda nchini Kenya kutumbuiza, akitokea Kongo Brazzaville. Alikuwa nchini humo kwa mwaliko wa Pamela Olet wa Kampuni ya Melamani Productions.
Lengo kubwa la ziara yake ya wiki mbili nchini humo ilikuwa ni kueneza amani na kuwatumbuiza mashabiki wake kwa nyimbo zake zilizotia fora kama vile ‘Nakei Nairobi’, ‘Eswi Yo Wapi’ na ‘Nadina’ alizoimba na marehemu Tabu Ley aliyekuwa kiongozi wa Afrisa International.
Mbilia mara baada ya kuwasili alisema amefurahi kurudi jijini Nairobi baada ya miaka 16.

“Nawapenda sana mashabiki wangu wa Kenya kwa sababu wananionyesha upendo na wanafurahia nyimbo zangu,” alisema Mbilia Bel.
Aidha, katika ziara yake hiyo alikwenda kuzuru wafungwa wa jela ya wanawake ya Lang’ata mjini Nairobi.
Hakusita kumsifia marehemu Tabu Ley kwa kukuza kipaji chake akiwa mnenguaji, akapanda ngazi na akawa mwimbaji.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0767331200 na 0713331200