‘Sheria inakwaza vyombo vya habari na kuzidi kusinyaa’

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

MJUMBE wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), na katibu mstaafu wa jukwaa hilo Neville Meena amesema kuwa bado kuna ukakasi kwenye sheria ya vyombo vya habari ya mwaka 2016.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Kituo cha Radio cha Nyemo, jijini Dodoma leo Agosti 17,202 kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya sheria kwa vyombo vya habari.

Meena amesema kuwa kati ya eneo ambalo lina ukakasi kuwa ni matangazo ya serikali kuratibiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.

“Sheria hii inakwaza vyombo vya habari kwa kuwa ina changamoto inayochangia sekta vyombo vya habari kuzidi kusinyaa,”amesema Meena.

Hata hivyo amesema kuwa sheria ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016, ilikataliwa siku ya kwanza baada ya kusainiwa na kuanza kutumika kama mwongozo kwa vyombo vya habari nchini.

“Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipingwa na wadau wa habari siku moja baada ya kupitishwa ili kutumikaa. Si kwamba, hakukuwa na vitu muhimu kwa wanahabari, wadau waliona imebeba mitego na madhara mengi kwa wanahabari na vyombo vya habari.

‘‘Wadau wa habari wakiwemo UTPC, TAMWA, MISA-TAN, LHRC, TLS, Twaweza, Sikika, THRDC na wengine, walikaa pamoja na kuangalia madhara yanayoweza kutokea kutokana na sheria hiyo.

‘‘Tunashukuru hatua zilipofika kwa sasa. Rais (Ramia Suluhu Hassan) amekuwa na utashi wa kufanya mabadiliko lakini hata waziri aliyepo sasa (Nape Nnauye), mwelekeo wake ni huo,’’ amesema Meena.

Amesema, baada ya serikali kuona umuhimu wa kupitia sheria hizo, iliandaa maboresho na kupeleka kwa wadau kupitia.

Na kwamba, baada ya wadau kupata mapendekezo hayo, waliyapitia na kuongeza pia kupunguza huku wakipitia zaidi vifungu vingine vya sheria vilivyoonekana kuwa hatari kwa wanahabari kutekeleza majukumu yao.

‘‘Hata yale mapendekezo yaliyoletwa na serikali, nayo tuliyaangalia na kuyapitia kisha kukubalina na baadhi na kisha mengine kutokubaliana nayo.

‘‘Kimsingi kuna baadhi ya vipengele ni vigumu kutelekezwa kama sheria ilivyompa madaraka mtu mmoja kufungia chombo cha habari. Hii ni hatari sana,” amesema Meena.