Shikizo la Mkulo lilivyoanza
Baada ya barua hii ya METL waliojitoa muhanga, Msajili wa Hazina kwa niaba ya Katibu Mkuu, katika barua aliyoiandika Julai 5, 2010 na kusainiwa na Ridhinwani Masudi, alimwandikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC Mbajo, akimtaka atekeleze yaliyomo katika barua ya METL ama kwa kumuuzia kiwanja Na 10 kwa kumpatia njia ya kufika kwenye kiwanja chake Na 11. Barua hii ina Kumb. TYC/A/290/13.

Mkulo alipoona agizo lake halijatekelezwa kwa miezi mitatu, ilipofika Oktoba 1, 2010 zikiwa ni siku 30 kabla ya uchaguzi, Wizara ya Fedha kupitia kwa Msajili wa Hazina, Geofrey Msella, kupitia barua yenye Kumb. Na TYC/C/180/85/59, iliandika barua yenye kichwa cha habari kisemacho:-

Yah: Uuzwaji wa Kiwanja Namba 10 Nyerere Road kwa Mohammed Enterprises Tanzania Limited. Barua hiyo iliendlea kusema: “Tafahdali, rejea maelekezo ya Wizara ya Fedha na Uchumi kuhusiana na mchakato wa kutatua suala la maingiliano kati ya DRTC Trading Company Limited na METL.

“Wizara ya Fedha na Uchumi ingependa kupata taarifa ya utekelezaji wa suala la Mohammed Enterprises Limited la KUUZIWA kiwanja Na. 10 Nyerere Road ili kumuwezesha kupata njia ya kuingilia kwenye Godowns zake bila kupitia Kiwanja Na. 192 Nyerere Road kinachomilikiwa na DRTC Trading Company Limited.

“Pamoja na kukutaka kumaliza mzozo wa siku nyingi uliopo, unatakiwa pia kuhakikisha kwamba wote waliouziwa maeneo wanapewa hatimiliki kwa maeneo yao husika.

“Nashukuru kwa ushirikiano wenu.
G. M. K. Msella.
Kaimu Msajili wa Hazina”

CHC baada ya kupata barua hiyo walifanya uthamini na waliwaeleza Hazina kuwa kumuuzia Mohammed Enterprises kiwanja hicho ilikuwa ngumu, kwani kulikuwapo na kesi mahakamani, lakini pia kwa kufuata sheria ya ununuzi wa umma, ilibidi kutangaza kiwanja hicho na kuwashindanisha wazabuni.

Hata hivyo, shinikizo lilizidi kuwa kali ikabidi Bodi ya Wakurugenzi wa CHC ikutane Aprili 2, 2011. Tena walikutana siku ya Jumamosi, ambapo walikutana wajumbe wa Bodi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi wakati huo, Profesa Hamisi Mahigi, Geoffrey Msella, ambaye ni Msajili wa Hazina, Dk. Raphael Chegeni, Aloyce Kimaro na Alhaj Shaweji Abdallah.

Watendaji waliohudhuria kikao hicho ni Metusela Mbajo (Ag. DG – CHC), Joseph Hellela, Albert Semng’indo, Dome Masolosha na Germana Ibreck.

Ajenda ilikuwa ni kujadili uuzaji wa Kiwanja Na 10. Kikao kilipokea taarifa ifuatayo:- “Moja, kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu wa kutokuwa na barabara ya kuweza kufika katika Kiwanja Na 11 kinachomilikiwa na METL bila ya kupitia katika Kiwanja Na. 192 kinachomilikiwa na DRTC.

“Mbili, METL amekuwa akitumia barabara inayopita katika kiwanja cha DRTC ili kufika katika maghala aliyouziwa na Serikali kupitia PSRC; tatu, hali hii imezua mgogoro kati ya DRTC na METL na pia kuihusisha Serikali; nne, Kufuatia uchambuzi kuhusu mgogoro huu, Waziri wa Fedha alishauriwa akubali na akaagiza CHC kukiuza kiwanja Na. 10 kwa METL kwa bei ya soko na kwa kuzingatia sheria na taratibu; na tano, agizo hilo linalenga kutatua mgogoro uliopo kati ya DRTC na METL.”

Baada ya wajumbe kupokea taarifa hiyo na kuijadili, Bodi ya Wakurugenzi iliamua yafuatayo:- “Bei ya Kiwanja kwa METL iwe ni ile iliyobainishwa katika “valuation” kama thamani ya soko inayozingatia kutoa njia ya barabara; mbili, Serikali isihusike tena na mgogoro wa barabara kati ya METL na DRTC mara baada ya METL kuuziwa kiwanja Na. 10; tatu, Kiwanja husika kiuzwe haraka ili Serikali iondokane na hasara inayotokana na mgogoro uliopo kati ya DRTC na METL.

“Tatizo la kisheria kati ya Serikali na Noble Azania Food Limited kuhusu ukodishwaji wa kiwanja hicho litakuwa limetatuliwa kwa sababu METL amekubali kuchukua matatizo yote (all encumbrances) yanayohusu kiwanja husika; tano Waziri wa Fedha ashauriwe kuhusu maelezo ya kikao ili kupata ushauri/uamuzi wake kulingana na mapendekezo ya Bodi na mwisho, menejimenti ishughulikie na kumaliza suala hili haraka iwezekanavyo.”

By Jamhuri