Bodi yawasiliana na Mkulo
Baada ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Bodi Profesa Mahigi alimpigia simu Mkulo siku hiyo ya Aprili 2, 2011 na Mkulo akamwambia wakutane Morogoro kwani alikuwa anaelekea bungeni Dodoma.

Baada ya kauli hiyo, Profesa Mahiga na Mbajo walifunga safari na kwenda Morogoro. Walikutana katika Hoteli ya Morogoro na Mkulo akawaagiza wauze kiwanja hicho kwa Mohammed Enterprises.

Kutokana na maagizo hayo yalikuwa ya mdomo, Mbajo alimuomba Mwenyekiti wa Bodi amwandikie kwa maandishi maagizo hayo, naye akamwandikia hivi:-

Yah: Maagizo ya Bodi ya Ufafanuzi wa Waziri wa Fedha, Mh. Mustafa Mkulo (MB).

“Tafadhali rejea mazungumzo ya kikao cha Bodi ya tarehe 2/4/2011 ambapo Bodi ilielekeza kwamba Shirika/Mwenyekiti wa Bodi (CHC) lipate ufafanuzi kutoka kwa Mh. Waziri wa Fedha kuhusu bei ya Soko/ya mthamini.

“Mimi kama Mwenyekiti wa Bodi na wewe kama Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC tulionana na Mh. Waziri wa Fedha, akafafanua kuwa katika mazingira ya kiwanja Na. 10, bei inayopaswa kutumika ni ya mthamini wa kiwanja na hakuna haja wala umuhimu wa kutangaza.

“Kwa sababu Mh. Waziri wa Fedha amefafanua hilo, ninakuelekeza kwamba utekeleze uamuzi wa Bodi wa kumuuzia kiwanja Na. 10 METL kwa masharti kwamba yeye atahusika na matatizo yote ya kiwanja hicho bila kuhusisha serikali. Na kwamba yeye (METL) anauziwa kiwanja tu bila mashine/mitambo iliyopo ndani ya jengo.

“Tafadhali tekeleza.

Asante.”

Mkulo amkwepa CAG

Kutokana na barua hii, katika ukaguzi maalumu uliofanywa na CAG, Ludovick Utouh, ndani ya CHC, Utouh alitaka kumhoji Mkulo hivyo akampigia simu kuomba miadi au kupanga utaratibu wa jinsi ya kukutana naye, lakini badala yake kusubiri aandikiwe barua ya kuhojiwa mara tu alipopigiwa simu na CAG Mkulo alichachawa.

Haraka haraka aliandika barua kinyume na taratibu za Serikali yenye Kumb. Na. TYC/B/70/2/03 na kuisaini yeye mwenyewe Mkulo huku akiigonga mihuri minne ya SIRI. Barua hiyo ya Oktoba 8, 2011 ilisema hivi:-

“Yah: Ukaguzi wa Consolidated Holding Corporation

 

“Tafadhali rejea mazungumzo yetu ya simu (UTOUH/MKULO) ya tarehe 07/10/2011 na ujumbe wa simu (SMS Message) wa tarehe 05/10/2011.

“Napenda kuthibisha niliyoyasema kwenye simu, “kwa maandishi” kwamba mimi kama “Waziri wa Fedha” sijawahi kutoa KIBALI kwa Mwenyekiti wa Bodi ya CHC, kumpa madaraka ya kuuza kiwanja au nyumba zinazomilikiwa au kutunzwa na CHC bila kufuata taratibu za zabuni au sheria ya manunuzi. Kama Mwenyekiti wa Bodi aliamuru Kaimu Mkurugenzi Mkuu na Bodi ya Wakurugenzi kuuza kiwanja cha Shirika bila kufuata taratibu za zabuni, alifanya hivyo kwa ridhaa yake mwenyewe na si kwa maagizo ya Waziri wa Fedha.

“Wizara ya Fedha ina utaratibu maalumu wa kushughulikia masuala yote yanayohusu mashirika ya umma. Kisheria huanzia kwa Msajili wa Hazina, kupitia kwa Katibu Mkuu – Hazina (PST/PMG) hadi kumfikia Waziri wa Fedha kwa uamuzi. Hivyo utaratibu uliotumiwa na Mwenyekiti wa Bodi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC ni kinyume na kanuni za utendaji kazi ndani ya Wizara ya Fedha na pia ni kinyume na kanuni za manunuzi.

“Nakushukuru sana kwa kunijulisha jambo zito ambalo sikuwa nikilifahamu. Natumaini kwa maelezo haya ya maandishi, ofisi yako sasa inaweza kukamilisha ukaguzi wa CHC.

“Mustafa Haid Mkulo (Mb.) Waziri wa Fedha.”

Barua hiyo kama zilivyo nyingine, ilipelekwa nakala Ikulu, CHC na kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina.

Kinachosikitisha, tangazo ambalo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ramadhani Khijjah ametoa magazetini Aprili 28, 2012 kumsafisha Mkulo pamoja na mawasiliano yote hayo na maelekezo kutoka katika wizara yake bila kutaja vikao alivyokutana na Profesa Mahigi na Mbajo, anasema halijui suala hilo. Je, nani mkweli, ni Mkulo au nyaraka rasmi zilizopo kwenye majadala ya serikali zinazoonyesha ushiriki wa Mkulo katika kushinikiza METL auziwe kiwanja Na. 10?

Ripoti ya CAG inasema Mkulo ameingilia mchakato wa uuzwaji wa kiwanja hiki, ila wizara yake inakanusha ripoti hii, pamoja na maelezo haya yasiyotiliwa shaka.

By Jamhuri