Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Mbunge wa Jimbo la Ubungo,Kitila Mkumbo amewashauri wadau wa habari kueleza hoja zenye tija kuhusiana na kupendekeza kwa baadhi ya vifungu vya sheria ya habari kuomba kubadilishwa.

Mkumbo ameyasema hayo jijini Dodoma alipozungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na mchakati wa mabadiliko ya sheria hiyo iliyotungwa 2016.

“Ni vyema wadau wa habari wakajipanga pindi watakapoitwa na kamati husika ya Bunge kutetea mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari kwa kutoa hoja nzito,” amesema.

Dk.Kitila amesema kuwa wadau wa habari watakapokuja kwenye kamati ni vizuri wakawa na hoja za msingi za kutaka sheria ya huduma za habari kuboreshwa.

“Unafahamu kwenye kamati ndio wadau wanapata nafasi ya kutoa hoja zao kwanini wanataka baadhi ya vipengele vifanyiwe marekebisho,” amesema Prof. Kitila.

Akizungumzia mchakato huo Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema, ingawa mpaka sasa hajajua wakati ambao mapendekezo hayo yatafikishwa bungeni, lakini bado ana matumaini kwamba safari ya mabadiliko hayo haitaishia njiani.

Balile amesema, serikali bado inaonesha kuwa na dhamira njema ya kufanya mabadiliko.

“Waziri wa Habari ndiye mwenye kujua lini watapeleka bungeni muswada lakini sisi wadau tumepewa fursa ya kutoa maoni yetu.

“Tumeona dhamira njema ya serikali hadi hivi sasa, tukiendelea hivi nadhani huko tuendako tutashirikiana vizuri kwa masilahi ya Taifa letu,” amesema.

By Jamhuri