Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Rukwa

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi, Catherine Mashalla ameunganishwa na washtakiwa wengine saba katika kesi ya uhujumu uchumi na kufanya idadi ya washitakiwa katika kesi hiyo kufikia 14.

Mashalla ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, ameunganishwa katika shauri hilo namba 5 la mwaka 2023, ambapo wamesomewa mashitaka 153, ikiwemo utakatishaji wa fedha, kuunda genge la uhalifu na kughushi malipo kwa njia ya mtandao kinyume na utaratibu.

Mshtakiwa huyo alikishwa jana Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rebeca Mwalusako, upande wa Jamuhuri ukiongozwa na mwendesha mashitaka wa TAKUKURU, ulieleza kuwa kesi hiyo mara ya kwanza ilitajwa mahakamani hapo Agosti 22, 2023 ikiwakabili washitakiwa saba.

Baada ya kusomewa mashtaka watuhumiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo haina mamlaka ya kuendesha kesi za uhujumu uchumi. Kesi imeahirishwa hadi Machi 28, mwaka huu itakapotajwa tena.