MWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru anatarajiwa kuzikwa Jumatatu Februari 5, 2018 katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa kamati ya maziko ya mwanasiasa huyo, Omary Kimbau amesema  Kingunge atazikwa saa tisa alasiri. Hata hivyo, amesema leo Ijumaa Februari 2,2018 kuwa utaratibu na mipango mingine inaendelea kufanyika.
Kingunge amefariki dunia leo alfajiri akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Alikuwa akiuguza majeraha baada ya kung’atwa na mbwa mwishoni mwa mwaka jana nyumbani kwake.
Mpwa wa Kingunge, Tony Mwiru amesema familia inapitia kipindi kigumu kwa kuwa hivi karibuni wamempoteza mama yao, Peras. Enock Mwiru ambaye ni mdogo wa marehemu na mtangazaji wa zamani wa iliyokuwa Redio Tanzania (RTD),  amesema  Kingunge alikuwa kiunganishi cha familia.
Mabalozi Juma Mwapachu na Ali Mchumo waliowahi kufanya kazi na Kingunge wamefika nyumbani kwa marehemu Kijitonyama kuhani msiba huo.