Na Mwandishi Wetu,Jamhurimedia

Serikali imesema itasimamia na kulinda uhuru wa kujieleza na haitoingilia kwenye uhuru wa vyombo vya habari.

Pia inataka kuwa mlezi wa uhuru wa kujieleza na haitaki kuingilia biashara ya vyombo vya habari.

“Inachotaka ni kuwa mlezi wa uhuru wa kujieleza na tunataka wamiliki wa vyombo vya habari, waendeshe biashara zao kama ilivyo kwa tasnia nyingine kama wanasheria, madaktari na wengine” amesema Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akizungumza na vyombo vya habari leo Februari 16, 2023 jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza ziara yake katika Kampuni ya Mwananchi Communication.

Nape amesema kuwa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari yaliyowasilishwa bungeni taarehe 10 Februari 2023, yanalenga kuimarisha uhuru wa kujieleza nchini.

“Serikali itasimamia na kulinda uhuru wa kujieleza. Itahakikisha inafanya kila linalowezekana kulinda haki hiyo,” amesema Nape.

Nape amesema,wakati ilipotungwa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016, kulikuwa na vilio vingi.

“Tusingeweza kuendelea na vilio hivyo, hivyo tumependekeza baadhi ya mabadiliko kwenye sheria hiyo,” amesema.

Na kwamba, muswada huo ukipitishwa kwa taratibu za Bunge na kutiwa saini na rais kuwa sheria kamili,utasaidia kuleta mageuzi makubwa kwenye tasnia ya habari nchini.

Amesema,baada ya muswada kusomwa bungeni,sasa utakabidhiwa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ambapo itakuwa na jukumu la kuwaita tena wadau wa masuala ya habari kwa ajili ya kuwasikiliza, kisha kamati hiyo ya Bunge itapeleka maoni ya wadau bungeni kabla ya Bunge kuanza kujadili maoni ya serikali kuhusu sheria hiyo.

“Tulifanya mazungumzo ya kutosha kwa mwaka mzima kati ya serikali na wadau juu ya maboresho ya ile sheria, na yale tuliyokubaliana, tumeyazingatia kama serikali kwenye mapendekezo yetu bungeni,” amesema Nape.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) Bakari Machumu, amesema, mchakato kuelekea sheria hiyo, umekuwa wa majadiliano zaidi kati ya serikali na wadau wa habari.

“Kuna mapendekezo ambayo tuliyapeleka, yamesomwa. Kwa hiyo, tunachoangalia kwa sasa ni kwenda mbele kujua nini kimewekwa na kitajadiliwa kwa njia ipi” amesema Machumu.

By Jamhuri