Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amekitaka Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC)  kuhakikisha miradi ya biashara ya kaboni inayotekelezwa inaleta matokeo halisi na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi badala ya kujikita katika idadi kubwa ya miradi isiyo na tija.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo wakati akikagua mabanda ya maonesho ya Washiriki wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JINCC), Dar es Salaam, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesisitiza kuwa, badala ya kujivunia miradi 119 iliyo kwenye maandalizi, ni muhimu kuweka nguvu katika miradi michache iliyoiva na kuhakikisha inazalisha mapato kupitia biashara ya kaboni na kuchangia maendeleo ya Watanzania.

“Ni bora tushike mradi mmoja, tuhakikishe tunakimbia nao na manufaa yake yanaonekana kwa Mtanzania. Tufanye vitu kwa uhalisia,” amesisitiza Mhe. Ndejembi.

Mkutano huo wa COP12 umezikutanisha nchi 10 wanachama wa Mkataba wa Nairobi kujadili masuala ya uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.