Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo amechukua fomu ya kugombea Uenyekiti wa Ngome hiyo ikiwa ni kipindi chake cha pili, huku akijivunia rekodi ya utendaji wa kazi wake.

Nondo ambaye amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo leo Februari 20,2024 akiwa pamoja na Mgombea Mwenza wake, Nassor Ahmed Marhun amesema Ngome ya vijana haijawahi kuogopa, kukosoa na kupinga vitendo vyote vya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuminya demokrasia, uhuru wa kuongea pamoja na uhuru wa vyombo vya habari.

Nondo ambaye pia ni Waziri wa Vijana, Ajira na Kazi katika Baraza Kivuli la chama hicho, amesema katika kipindi kigumu ambacho nchi ilikuwa kwenye mtanziko wa kisiasa, Ngome ya Vijana ilisimama kidete na imara kuhami demokrasia na kuheshimu uhumu wa maoni.

“Huu umekuwa wajibu wetu wa kila siku kwenye utumishi, mimi na wenzangu ndani ya Ngome ya Vijana leo na hata kesho,” amesema Nondo.

Kuhusu utekelezaji wa vipaumbele alivyoahidi katika uongozi wake kwa kipindi kinachomalizika, amesema aliahidi kuifanya Ngome ya vijana kuwa chombo cha utetezi na kusemea masuala yote yanayohusu maslahu ya vijana nchini.

“Nimefanya kazi hiyo na viongozi wenzangu na tumeifanya Ngome kuwa sauti ya kusemea changamoto mbalimbali za vijana, ajira, uonevu, mikopo ya elimu ya juu.

“Tumefanya kazi hii kwa jasho na jitihada zetu zote na ndiyo maana Ngome ya Vijana ACT Wazalendo kuwa kimbilio la vijana nchini hasa wanapohitaji msaada wa utetezi na kusemewa, na mara nyingi sauti yetu imekuwa yenye nguvu kwa Serikali pindi tunapozungumza”amesema.

Kwa upande wake, Mgombea Mwenza wa Ngome ya Vijana, Nassor Ahmed Marhun amewaahidi vijana wa ACT Wazalendo kuwa endapo watachaguliwa wamejipanga kutafuta na kutetea ushindi wa chama chao katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa misingi ya haki kama vijana wazalendo wa Taifa hili.

“Niwahakikishie hatutoweza kukubali kuona ubakwaji wa demokrasia katika nchi yetu, tutasimama imara kuitetea nchi yetu na haki za vijana kwa ujumla. Na mpango kazi wetu ifikapo 2025 ni kuhakikisha ACT Wazalendo inashinda kwa kishindo kikubwa na kuongoza Serikali zote mbili, ya Muungano na Zanzibar.