Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia bibi mmoja aitwaye Malogi Luobela (75), Mkazi wa Kijiji cha Ikoho Wilaya ya Mbeya Vijijini kwa tuhuma za kumuua mjukuu wake aitwaye Vision Erick mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mitano kwa kumkata kwa jembe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzagani, alisema kwamba Agosti 31, 2023 majira ya saa 4:30 asubuhi huko Kitongoji cha Mapinduzi, Kijiji cha Ikoho, Kata ya Maendeleo, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya Vijijini, mtoto huyo ambaye ni marehemu, mwaka mmoja na miezi mitano alifariki dunia baada ya kukatwa kwa jembe kichwani na bibi yake aitwaye Malogi.

Kamanda alisema chanzo cha tukio hili ni mtuhumiwa alikuwa anachimba udongo ili kukandika katika nyumba na ndipo wakati anaendelea mtoto huyu alitambaa hadi eneo hilo bila mtuhumiwa kumuona kutokana na hali yake ya uono hafifu [upofu] na ndipo alimkata kwa jembe kichwani na kusababisha kifo chake.

Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamsaka dereva wa Gari yenye namba za usajili T.436 CGD aina ya Mitsubishi Canter mali ya kampuni ya Mainland Pharmacy Center aitwaye Khadhar Adam (28), Mkazi wa Mkoa wa Katavi – Mpanda, mwenye asili ya Kisomalia kwa tuhuma za kumgonga kwa Gari askari wa Kikosi cha usalama barabarani WP.2645 S/SGT Zaina akiwa katika majukumu yake.