Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imeweka kipaumbele kupata suluhisho la kudumu la umeme Zanzibar kwa kuongeza uzalishaji wa ndani, kupanua matumizi ya nishati mbadala na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji, ili kuongeza uhakika wa nishati na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nje.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 28 Oktoba 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Sono, Yeosu, Jamhuri ya Korea (Korea Kusini) alipokutana na uongozi wa WongWang Electric Power Corporation (WG Corporation), kampuni ya Korea Kusini inayojishughulisha na mifumo ya umeme na nishati mbadala.
Ameeleza kuwa Zanzibar bado inategemea umeme kutoka Tanzania Bara huku ikikabiliwa na upungufu wa umeme, hivyo Serikali inaendelea kuimarisha juhudi za kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi huo.
Katika mazungumzo hayo, wamejadili uwezekano wa kushirikiana katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati mbadala, pamoja na mifumo ya uzalishaji na uhifadhi wa umeme inayoweza kutumika katika visiwa vidogo na maeneo yaliyo mbali na gridi kuu.
WG Corporation imeeleza uzoefu wake katika miradi ya nishati mbadala, mifumo ya gridi ndogo za umeme, uhifadhi wa nishati na miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme, ikiwemo utekelezaji wa miradi visiwani.
Kampuni hiyo pia imeonesha utayari wa kutuma timu ya wataalamu Zanzibar kwa ajili ya kufanya tathmini ya mahitaji ya kiufundi na maeneo ya utekelezaji wa miradi, baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria.
Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kuondoka Yeosu leo tarehe: 28 Oktoba 2026 kuelekea Kisiwa cha Jeju, ambako atashiriki Jukwaa la 27 la Sera za Utalii kwa Visiwa (ITOP Forum 2026) litakalowakutanisha viongozi na wataalamu kutoka visiwa na maeneo wanachama kujadili utalii endelevu, ushirikiano wa visiwa na changamoto zinazokabili maendeleo ya maeneo ya visiwa.









