SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua kampeni ya Bureee Kabisaaa inayolenga kuwawezesha wateja kupata huduma za intaneti ya nyumbani, simu ya mezani, ruta, laini tatu za simu za mkononi na burudani bila malipo ya ziada, kwa kuzingatia masharti ya ofa hiyo.
Kampeni hiyo inalenga kupanua matumizi ya teknolojia ya kidijitali nchini na kuimarisha mawasiliano ya kifamilia kwa kuwawezesha wateja kupata huduma mbalimbali kupitia kifurushi kimoja cha Triple Hub kinachoanzia Sh70,000.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 28, 2026, Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Vedastus Mwita, amesema kampeni hiyo inalenga kuwawezesha Watanzania kupata huduma za intaneti kwa gharama nafuu na kuendelea kuwasiliana na familia zao kwa urahisi, wakiwa nyumbani au safarini.
Amesema kampeni hiyo imebuniwa kukidhi mahitaji ya wateja wanaohitaji huduma za intaneti zinazowawezesha kuendelea kuwasiliana bila usumbufu, bila kulazimika kununua vifurushi tofauti vya simu za mkononi.
“Tunatambua wateja wetu wanahitaji mawasiliano yasiyokatika, si tu wanapokuwa nyumbani bali hata wakiwa nje. Ndiyo maana tumezindua Triple Hub ili kurahisisha matumizi ya intaneti kote nchini,” amesema Mwita.
Ameeleza kuwa huduma hiyo inategemea mfumo wa Fiber Mlangoni Kwako, huku Triple Hub ikiunganisha intaneti, simu na burudani katika kifurushi kimoja.
Kwa mujibu wa Mwita, wateja watakaokidhi masharti ya kampeni hiyo watapatiwa simu ya mezani pamoja na ruta bila malipo, vitakavyowawezesha kutumia huduma za mawasiliano kulingana na kifurushi walichojiunga nacho.
Aidha, amesema kila mteja atakayekidhi vigezo atapata laini tatu za simu za mkononi kwa ajili yake na familia yake, zitakazomwezesha kutumia huduma za intaneti za TTCL hata anapokuwa nje ya nyumbani.
Mbali na huduma hizo, wateja watanufaika na T-Burudani, inayowawezesha kutazama filamu, tamthilia na maudhui mengine ya burudani kupitia vifaa vyao.
Mwita amesema wateja wapya wanaotaka kunufaika na kampeni hiyo wanapaswa kujaza fomu ya maombi ya kuunganishwa na huduma ya Fiber Mlangoni Kwako na kuchagua kifurushi cha Triple Hub cha Sh70,000 au zaidi.
Kwa upande wa wateja waliopo, amesema wanachotakiwa kufanya ni kuboresha vifurushi vyao vya sasa kufikia Sh70,000 au zaidi ili kunufaika na ofa hiyo kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa.
Amewataka wateja kutembelea maduka au ofisi za TTCL wakiwa na namba zao za huduma kwa ajili ya uhakiki na kukabidhiwa vifaa vinavyotolewa kupitia kampeni hiyo.
Kampeni hiyo inapatikana katika maeneo yenye mtandao wa TTCL, yakiwemo Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa na Unguja.
Mwita amewahimiza Watanzania kuchangamkia fursa hiyo ili kuimarisha mawasiliano ya kifamilia na kunufaika na huduma za intaneti ya kasi kuelekea mwisho wa mwaka.
“Tumezindua rasmi kampeni yetu ya Bure Kabisa ili wateja wafurahie huduma zetu za TTCL,” amesema.



