Rais Samia amesema Tanzania inahitaji Sheria Madhubuti kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na umiliki wa rasilimali.

Rais Samia ameyasema hayo leo kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika WiLDAF yaliyofanyika ukumbi wa Serena

Amesema licha ya takwimu kuonyesha kuwa asilimia kubwa ya wanawake wanajishughulisha na shughuli za uzalishaji, bado baadhi ya mila na desturi zinawafanya wanawake kuendelea kukandamizwa.

Rais Samia pia amesema Sheria ni nyenzo kuu ya ufikiwaji wa usawa wa kijinsia na usitawi wa wanawake hivyo kutoa kipaumbele kwa wanawake ni jambo la lazima ili kuleta maendeleo.

Vilevile, Rais Samia amesema ipo haja ya kufanya tahmini ya sheria zilizopo na kuona zina mchango gani kwa Watanzania na kuhakikisha kuwa zinakwenda ngazi za nchi ili ziweze kutambuliwa na kufahamika kwa wananchi .

Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa wito kwa Sheria kutungwa na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kurahisisha kutoa elimu kwa wananchi.

Rais Samia ameagiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu pamoja nabWasaidizi wa masuala ya Sheria kuwashirikisha wananchi na viongozi wa dini na kimila katika kuondoa vitendo vya udhalilishaji na ukandamizaji dhidi ya mwanawake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwapa Tuzo baadhi ya Waanzilishi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika WiLDAF pamoja na vyeti kwa wadau waliofanikisha maendeleo ya Shirika hilo kwenye Maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa Shirika hilo kwenye hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Oktoba, 2022
Bendi ya Bahati ikitumbuiza kwenye Maadhimisho ya miaka 25 ya Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika WiLDAF katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Oktoba, 2022.