Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kupitia Bia yake ya Serengeti Lite imezindua Tamasha la Serengeti Oktoba litakalofanyika Oktoba 21,mwaka huu Ufukwe wa Coco, Dar es Salaam.

Meneja wa Bia ya Serengeti Lite, Esther Raphael, amesema tamasha hilo linakusudia kusherekea tamaduni za kitanzania na litafanyika Oktoba 21, mwaka huu hapa nchini kisha Kenya, Uganda na Sudani Kusini.

“Oktoba Fest 2023 inatarajwa kuwa tukio la pekee linalounganisha watu mbalimbali ili kufurahia ladha, sauti na tamaduni za kipekee za Tanzania. Ni sherehe ya kipekee inayojumlisha vyakula, muziki na utamaduni za Kitanzania. Watu wanaweza kutarajia nakshi za kipekee kupitia ladha tofauti na vibanda vingi vitavyohudumia vyakula vitamu vinavyoakisi ladha mbalimbali za kitanzania.

Meneja wa Chapa wa Bia ya Serengeti Lite,Esther Raphael, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Dar es Salaam Septemba 20, 2023 kuhusu tamasha hilo linavyotarajiwa kufanyika. Kushoto ni Meneja Mawasiliano na Uendelevu wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Rispa Hatibu.

“Kuanzia vyakula vitamu vya kitamaduni hadi ubunifu wa kisasa wa mchanganyiko, Oktoba Fest ni tukio pekee la kitamaduni,” amesema.

Pia amesema kutakuwa na safu ya muziki wa tamasha hilo utakaokuwa na mchanganyiko wa midundo ya kitamaduni na kisasa inayoshirikisha wasanii mbalimbali wa Tanzania.

“Wasanii hawa watapanda jukwaani ili kuonyesha sauti zao za kipekee, kuonyesha uzoefu wa muziki usiosahaulika kwa wahudhuriaji,” amesema.

Aidha, amesema muziki, maonyesho ya dansi,sanaa na mitindo yatazingatia urithi wa kitamaduni wa Tanzania na kutoa uzoefu wa kusherekea utofauti wa kanda.

Naye Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, Aneth Rwehumbiza, amesema tamasha hilo si tu ni sherehe ya utamaduni lakini inalenga kuleta matokeo chanya kwa sehemu zote muhimu katika jamii yetu.

“Serengeti Breweries imejitoa kwa dhati kuleta matokeo chanya kwa jamii inayohudumia. Tamasha hili litawasaidia wajasiriamali na wasanii kupata ustawi katika nyanja zao zinazokuza ujasiriamali, ubunifu na uendelevu.

“Kama wadhamini wa tamasha hilo, Serengeti Breweries ina nia ya kuhamasisha utamaduni wa Mtanzania. Kutoka chakula, mitindo na sanaa, Oktoba Fest inalenga wasanii wachanga kwa kutoa jukwaa kwa vipaji vinavyoibuka ili kuonyesha ubunifu wao na ustadi wa mapishi, kukuza ujasiriamali na ubunifu,” amesema.

Vilevile amesema tamasha hilo litajumuisha michezo mbalimbali inayounganisha teknolojia na mila, kutoa mtazamo wa pekee juu ya utamaduni wa kitanzania.

Pia amesema tamasha hilo linachukua hatua muhimu kwa ajili ya kupunguza athari katika mazingira.

“Juhudi kama vile udhibiti na utupaji ovyo wa taka na mbinu endelevu zitawekwa ili kuhakikisha usafi wa mazingira katika tamasha hili,” amesema.

By Jamhuri