Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Serikaki ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya juhudi za makusudi kudhibiti mfumko wa bei hasa kwa bidhaa za chakula nchini.

Aidha, imetoa agizo kwa wafanyabiashara wote wa vyakula kupunguza bei ya sukari ambayo ushuru wake kwa Zanzibar ni mdogo zaidi kuliko popote dunuani.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipokutana na wafanyabiashara mbalimbali nchini, wazalishaji wanaoingiza bidhaa na mizigo na wadau wote wa biashara zikiwemo taasisi za Serikali na binafsi kujadili mustakbali wa bei za bidhaa hasa vyakula zinazopanda kila uchao.

Rais Dk. Mwinyi amewaeleza wanafanyabiashara hao kuwa karibu na kuzungumza na Serikali wakati wote kunapotokea matatizo badala ya kuwapandishia bei wananchi kwani wao ni waathirika wakubwa.

Akizungumzia suala la fedha sarafu ya dola Rais Dk. Mwinyi alizitaka mamlaka husika kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara wa chakula ili kuwaondoshea wananchi usumbufu wa uhaba wa chakula nchini.

Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi amewataka wafanyabiashara hao kuangalia uwezekano wa kuagiza bidhaa kwa pamoja na kuingiza nchini kwa wakati ili kuepuka gharama za usafirishaji na kuchelewa kuingiza vyakula nchini pamoja na kuwapa agizo la kushusha vyakula Pemba.

“Lazima kutafutwe njia ya kushushia vyakula moja kwa moja Pemba, mshirikiane kuchukua meli kutoka bandari ya Malindi hadi Pemba, kutafutwe ufumbuzi kwa njia yoyote ili kupunguza gharama za bidhaa madukani” amesisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Akizungumzia mabadiliko kwa Shirika la Bandari la Zanzibar Rais Dk. Mwinyi ameeleza mabadiliko yoyote yanachangamoto zake, hivyo aliwataka wafanyabiashara hao kutoa ushirikiano kwa uwekezaji mpya wa bandari hiyo na kuuagiza uongozi wa Shirika la Bandari kusimamia changamoto zinazojitokeza kwa kipindi hiki cha awali cha mkataba na wawekezaji.