Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali inachukua hatua katika kuimarisha uwezeshaji wanawake kiuchumi pamoja na kuongeza uelewa kuhusu mifuko ya maendeleo inayowanufaisha wanawake.
Akizungumza juzi bungeni jijini Dodoma, Mahundi alisema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanapata taarifa na kunufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), ikiwa ni pamoja na kushirikiana na taasisi za fedha na wadau wa maendeleo kutoa mafunzo ya ujasiriamali na uendeshaji wa biashara kupitia makongamano ya kikanda.
“Serikali itaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, TAMISEMI pamoja na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuhakikisha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yanapatiwa mafunzo na fursa za mikopo nafuu.” amesema Mhe. Mahundi.
Katika swali lingine, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifuko iliyopo badala ya kuanzisha mipya, ikiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake unaotoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali.
“Kupitia ushirikiano na Benki ya Dunia, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanza utoaji wa mikopo kupitia mradi wa PAMOJA, hatua itakayopanua wigo wa wanawake kunufaika na fursa za kiuchumi”. alisema Mahundi.
Alieleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha wanawake wanajengewa uwezo wa kiuchumi na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

