Mwanafunzi wa Tanzania aliyekuwa akisoma nchini Afrika Kusini ameuwawa kikatili Ijumaa nchini humo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mindi Kasiga amesema wizara inafanya mawasilianao na ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ili kubaini undani wa suala hilo.

Alisema wizara inafuatilia kujua chuo alichokuwa akisoma, siku ya tukio hilo na masuala yote muhimu kuhusiana na kifo hicho.

Taarifa hizo zilidai kuwa mwanafunzi aliyejulikana kwa jina la Baraka Nafari aliyekuwa akichukua Shahada ya Uzamivu (PHD) katika Chuo Kikuu cha Johannesburg (UJ) aliuawa mapema Ijumaa Februari 23, mwaka huu kwa kugongwa na gari mara mbili na kubamizwa kwenye ukuta na baadaye kushambuliwa kwa visu.

Kwa mujibu wa habari hizo za mtandao kamera za usalama za CCTV za chuo hicho zilionesha Baraka na mwanafunzi mwenzake wakikimbia kujiokoa wakati wanaume wawili kwenye teksi wakiwaandama.

Pia kamera hiyo iliendelea kumuonesha dereva wa teksi akimgonga kwa makusudi mwanafunzi huyo kwenye uzio wa makazi ya chuo hicho yaliyoko Auckland Park na kumuua.

Taarifa hizo zimeongeza kuwa dereva wa gari hilo alikamatwa na polisi kwa kuendesha bila leseni, lakini baadaye aliachiwa huru bila kufunguliwa mashtaka yoyote.

By Jamhuri