Sonona imegharimu maisha ya Rapa Riky Rick

DAR ES SALAAM

Na Christopher Msekena na mitandao 

Tasnia ya burudani Afrika Kusini bado imo katika simanzi ya kuondokewa na rapa mwenye mafanikio na mshindi wa tuzo mbalimbali, Riky Rick, aliyefariki dunia kwa kujinyonga Jumatano asubuhi ya wiki iliyopita.

Riky anayetajwa kuwa ni miongoni mwa marapa tajiri Afrika Kusini alipoteza maisha akiwa anakimbizwa hospitalini na uongozi wake ulimkuta akiwa amejinyonga kwa kamba nyumbani kwake huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni sonona (depression). 

Tukio hilo bado linaendelea kuchukua sura mpya, pia ni mkasa wa pili kwa mwaka huu baada ya mwigizaji gwiji nchini humo, Patrick Shai, naye kujiua kwa mtindo huo Januari 22, mwaka huu jijini Johannesburg.

Sonona imeendelea kutajwa kama sababu kubwa inayowatesa watu maarufu kwenye tasnia ya burudani nchini humo huku baadhi yao wakipata na tatizo la afya ya akili hadi kufikia hatua ya kujiua.

Riky hakuwa na makundi kama walivyo mastaa wengi nchini humo, msiba wake umepokewa kwa mshtuko mkubwa na wasanii wenzake na mashabiki kwa ujumla, hasa ukizingatia siku moja kabla ya kifo chake alikuwa ametoka kusaini dili nono la ubia na African Bank.

Hivyo kwake fedha haikuwa shida ndiyo maana mashabiki wamekuwa wakihoji tatizo ni nini hadi akafikia hatua ya kujiua angali bado kijana mdogo na mwenye mafanikio makubwa.

Aidha, katika kile kinachotajwa kuwa rapa huyo hakuwa sawa na mkewe Bianca na alikosolewa vikali na mashahabiki wake mtandaoni Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day) baada ya kuposti mtandaoni video akicheza muziki na mke wake, lakini jambo la kustaajabisha mpenzi wake huyo hakuonyesha kufurahia.

Miongoni mwa marafiki wa karibu wa Riky ambaye pia naye ni rapa AKA, ameweka wazi kuwa kuna umuhimu wa wanaume nchini humo kuwa na jukwaa la kuzungumza mambo yao, kwa sababu kuna mengi wanapitia yanayowapa msongo mkubwa wa mawazo hadi wengine wanaishia kujiua.

“Nimeshuhudia matukio matano ya watu wakijiua, miongoni mwa hao, wanne ni wanaume. Riky amekulia sehemu yenye fedha lakini imetokea hivi, tunapita katika mambo magumu na tunakosa watu wa kuongea nao licha ya kuwa na fedha na mafanikio bado wanaume hatuko sawa, ona tunavyochukua maisha yetu wenyewe takwimu zinatisha,” anasema rapa AKA.

Riky Rick ni nani?

Jina lake halisi ni Rikhado Makhado a.k.a Riky Rick ambaye ni rapa, mwimbaji na mtunzi wa nyimbo humo Afrika Kusini aliyezaliwa mjini Natal miaka 34 iliyopita na kufanikiwa kuanzisha Lebo yake ya Cotton Club Records huku akiwa ni miongoni mwa wasanii katika kundi la Boyz N Bunks.

Katika muziki alianza kuvuma mwaka 2014 baada ya kuachia wimbo wake ‘Nafukwa’ uliomtambulisha na kumpa mashabiki wengi kabla hajaachia albamu yake ya kwanza ‘Family Values’ iliyobadilisha kabisa maisha yake kwa kuuza viwango vya Platinum.

Riky alifanikiwa kuwapata mashabiki wa pande zote za mahasimu nchini humo – yaani marapa Cassper Nyovest na AKA kwa sababu licha ya bifu la hao wawili yeye alikuwa na urafiki na wote.

Japokuwa alikuwa rafiki zaidi na Casper Nyovest na urafiki wao uliingia zaidi katika kazi, kwa sababu walishirikishana   kwenye ngoma kibao huku kila mmoja akimshirikisha mwenzake, hivyo kufanya urafiki wao udumu zaidi.

Licha ya wawili hao kutofautiana miaka mitatu iliyopita ila katika msiba huo Cassper ameonyesha kuguswa kwa kuchapisha picha yake mtandaoni akiwa pamoja na Riky Rick na kusema: “Labda hii ndiyo picha ninayoipenda zaidi. Kuna hadithi ya kuchekesha sana kama mwanamume huwa sifurahii mwanamume mwingine akinigusa au kibaya zaidi kuwa nyuma yangu. 

“Kwa hiyo Riky aliponijia nyuma yangu katikati ya mahojiano, nilichofanya ni kugeuka na kuuliza nani wewe, lakini niliposikia sauti yake ilibidi nicheke na kuwa mpole, kwa sababu ni yeye. Sikumbuki alichosema kwenye mahojiano haya lakini najua alikuwa akionyesha upendo kama alivyokuwa akifanya siku zote. Bado siko tayari kukubaliana na tukio hili lakini kila nilichoshiriki na Riky kilikuwa cha kweli na sote tulijua.”

Utajiri wake

Rapa huyu alikuwa ni miongoni mwa wasanii wenye mafanikio makubwa na kwa mujibu wa vyanzo vya habari Afrika Kusini, Riky alikuwa na jumla ya utajiri wa dola milioni 30 za Marekani.

Alikuwa akimiliki Lebo ya Cotton Club Records yenye uhusiano na Sony Music pamoja na Kampuni yake ya mavazi ya Cotton Fest inayoshirikiana na Puma. Pia alikuwa na nyumba na magari ya kifahari yenye thamani ya dola milioni tano za Marekani.

Familia 

Riky ambaye hadi anafariki dunia alikuwa anatamba na wimbo ‘Sondela’, amekuwa mfano wa kuigwa hasa linapokuja suala la familia, kwa sababu amekuwa akionekana kama mume bora kwa mkewe Bianca au Aunt B na baba bora kwa watoto wake wawili (wa kike na wa kiume).

Mazishi

Kamati ya mazishi ya rapa huyo imeweka wazi kuwa Riky atazikwa leo Jumanne, Machi Mosi, mwaka huu jijini Johannesburg huku wakitarajia msiba huo uhudhuriwe na watu wachache.