Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia,Songea

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma limeweka makubaliano ya pamoja na wafanyabiashara wa vyuma chakavu mkoani humo katika suala zima la kulinda miundombinu mbalimbali iliowekwa na Serikali kwa maendeleo ya wananchi ikiwemo ya umeme ili isihujumiwe.

Makubaliano hayo yamefanyika kwenye kikao cha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa vyuma chakavu toka Wilaya zote za mkoa huo wakiwemo na Viongozi wa Jeshi la Polisi na watu wa mazingira toka NEMC.

Bw. Obasanjo Nniwako, mkaguzi wa Mazingira -NEMC Kanda ya kusini akitoa mada juu ya upatikanaji wa vibali na Leseni za kufanya biashara ya vyuma Chakavu, kwenye kikao cha wafanyabiashara wa vyuma Chakavu na Tanesco mkoani Ruvuma.

kikao hicho ambacho kimejadili juu ya mkakati wa kupambana na hujuma za miundombinu ya Umeme Mkoani Ruvuma ambapo toka January hadi Juni mwaka huu hali imekuwa mbaya kwa kuharibiwa miundombinu ya umeme na kulisababishia shirika hasara.

Akizungumza kwenye kikao hicho Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoani Ruvuma mhandisi Malibe Boniphace amesema kuwa wameamua kufanya kikao hicho na kuwashilikisha wadau hao baada ya kubaini uwepo wa uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya Tanesco ambayo imekuwa ikisababisha hasara kwa Serikali .

Boniphace akizungumzia suala la miundombinu ya umeme amesema kuwa wamekuwa wakikata nyaya za umeme , vyuma ambapo wateja wakubwa wa vifaa hivyo ni baadhi ya wanunuzi wa vyuma chakavu .

Baadhi ya washiriki wa kikao cha wadau juu ya mkakati wa kupambana na hujuma za miundo mbinu ya umeme mkoani Ruvuma kilichafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Tanesco Manispaa ya Songea.

Amesema kuwa kufuatia kikao hicho kutasaidia kushilikiana kuwafichua wahalifu ambao wamekuwa wakiiharibu miundombinu hiyo na kuwafanya baadhi ya Wananchi kukosa huduma za Umeme pamoja na kuisababishia hasara Serikali.

Kwa upande wake mkuu wa Oparesheni Kamishina msaidizi wa Polisi ACP Ramia Mganga amesema kuwa jeshi la Polisi lipo imara kupambana na waharifu wa miundombinu hiyo kwa kuwasaka kila sehemu patakapo kuwa kumefanyika uharifu .

Kamishina msaidizi Mganga ambaye amemwakilisha kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma ACP Marko Chiliya amesema kuwa baadhi ya waharibifu wa miundombinu ya Umeme ,Maji na ya barabara wameweza kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Amesema kuwa kuanzia sasa makubaliano yaliofikiwa na wafanyabiashara wa vyuma chakavu itasaidia kupunguza wimbi la waharifu hao kwa kuwa wote watakuwa walinzi wa miundombinu hiyo.

Naye Afisa usalama usimamizi kanda ya kusini Richard Damas amesema kuwa vikao hivyo vitafanyika Nchi nzima kwa kuwa Serikali karibu kila mkoa kuna miradi mbalimbali inafanyika ikiwemo ya Tanesco .

Mhandisi Albano Sembua meneja wa mradi wa msongo wa kilowati 220 Songea hadi Tunduru, akielezea athari za kuhujumu miundo mbinu ya umeme hasa kwenye nguzo za vyuma na Transformer.

Damas amesema kuwa kama wanunuzi wa vyuma chakavu wakipatiwa Elimu na kukaa vikao vya pamoja miundombinu mbalimbali ikiwemo ya Umeme haitaharibiwa kwa kuwa wote watakuwa sehemu ya walinzi wa miundombinu hiyo.

Naye mmoja wa washiriki wa kikao hicho ,Kadoda Mbalale ambaye pia ni mfanyabiashara wa vyuma chakavu amesema kuwa kupitia kikao hicho wamepata uelewa juu ya kujiepusha kununua vyuma chakavu vinavyotokana na miundombinu ya Serikali.

By Jamhuri