Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya Serengeti Girls kwa kuibamiza Les Bleues ya Ufaransa mabao 2-1 katika michuano ya Kombe la Dunia kwa Wasichana chini ya Umri wa Miaka 17 (U17) katika mchezo wa Kundi D Uwanja wa Jawaharlal Nehru, Margao, Goa nchini India

“Hongereni vijana wangu Serengeti Girls kwa ushindi wa 2-1 mlioupata leo (jana) dhidi ya Ufaransa. Nawaomba Watanzania tuendelee kuwaombea na kuwatia hamasa vijana wetu ili waendelee kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya miaka 17 huko India,”ameeleza Rais Samia.
Mabao ya Serengeti Girls yamefungwa na Diana Mnally dakika ya 16 na Christer Bahera dakika ya 56 kwa penalti.

Ufaransa walipata bao la kufutia machozi dakika ya 75 likifungwa na Lucie Calba ,Serengeti girls watacheza na Canada Siku ya Jumanne huku wakihitaji ushindi au sare ili waweze kutinga robo fainali ya Michuano hiyo.

Ikumbukwe Serengeti Girls ilianza vibaya michuano hiyo kwa kuchapwa 4-0 na Mabingwa watetezi, Japan.

By Jamhuri