Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Tanzania imepata fursa ya kupokea wageni zaidi ya 600 kama mwenyeji wa kongamano la Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) barani Afrika (SACCA CONGRESS 2026) kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika usimamizi na uendelezaji wa vyama hivyo, pamoja na jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta ya ushirika wa kifedha nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kongamano hilo, Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Collins Nyakunga, amesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi wa vyama vya ushirika na mazingira yanayowezeshwa na Serikali ikiwamo kuimarisha utendaji wa vyama vya akiba na mikopo.
” TCDC iliyopo chini ya Wizara ya Kilimo, ina jukumu la kusimamia na kuendeleza vyama vya ushirika nchini ili kuhakikisha vinazingatia taratibu na wanachama wanakuwa na imani na taasisi hizo” ameshasema.
Akifafanua zaidi amesema vyama vya ushirika nchini vinaunganisha sekta mbalimbali, ikiwamo kilimo, mifugo, uvuvi na huduma za kifedha kupitia SACCOS, ambazo hutoa huduma za akiba na mikopo kwa wanachama wake.
Amesema kongamano hilo linalosimamiwa na Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo Afrika (COSCA) ni fursa kwa Tanzania na washiriki wengine kujifunza mbinu bora za kuimarisha usimamizi wa vyama hivyo na kuongeza manufaa kwa wanachama.
” Kongamano hili limewakutanisha wadau zaidi ya 600 kutoka Tanzania na nchi mbalimbali za Afrika kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya kuboresha huduma za kifedha kupitia vyama vya ushirika.”amesema Nyakunga.
Pamoja na mambo mengine, hoja zinazotarajiwa kujadiliwa ni, namna ya kuhakikisha wanachama wananufaika na mikopo wanayopata kupitia SACCOS zao, pamoja na kuweka mazingira yatakayowavutia watu wengi zaidi kujiunga na vyama hivyo.
Aidha, amesema kongamano hilo limepangwa kufanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 16, huku ufunguzi rasmi ukitarajiwa kufanyika Oktoba 15 na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye katika maelezo yake amemtaja kuwa Anna Kilimo Mgululwa Mkichemba.
Amesema Tanzania itaendelea kutumia fursa hiyo kuimarisha sekta ya ushirika wa kifedha kwa kujifunza uzoefu wa nchi nyingine na kuboresha mifumo ya usimamizi ili vyama vya SACCOS viendelee kuwawezesha wanachama kiuchumi.





