KWA mara nyingine tena waokoaji wanatafuta watu waliokwama chini ya vifusi baada ya matetemeko mawili mapya ya ardhi kuikumba Uturuki na kuua takribani watu watatu.

Matetemeko ya ukubwa wa 6.4 na 5.8 yalipiga kusini-mashariki karibu na mpaka na Syria, ambapo matetemeko hayo yaliharibu nchi zote mbili mnamo 6 Februari.

Matetemeko ya awali yalisababisha vifo vya watu 44,000 nchini Uturuki na Syria huku makumi ya maelfu ya wengine wakiachwa bila makazi.

Majengo yaliharibiwa na matetemeko hayo yaliporomoka katika nchi zote mbili siku ya Jumatatu.

Shirika la maafa na dharura la Uturuki linasema tetemeko hilo la 6.4 lilitokea saa 20:04 saa za ndani (17:04 GMT), na kufuatiwa na tetemeko la 5.8 dakika tatu baadaye.

Vifo hivyo vitatu vilitokea Antakya, Defne na Samandag, Waziri wa Mambo ya Ndani Süleyman Soylu aliiwataka watu kutoingia kwenye majengo yanayoweza kuwa hatari.Soylu alisema watu 213 pia wamejeruhiwa.

Ripoti kutoka mji wa Antakya zilizungumza juu ya hofu mitaani huku magari ya kubebea wagonjwa na wafanyakazi wa uokoaji wakijaribu kufika katika maeneo yaliyoathirika zaidi ambapo kuta za majengo yaliyoharibiwa vibaya yaliporomoka.

“Nilidhani dunia imepasuka chini ya miguu yangu,” mkazi wa eneo hilo Muna al-Omar aliliambia shirika la habari la Reuters, huku akilia akiwa amemshika mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka saba.

By Jamhuri