Mwanafunzi wa shule ya sekondari amemchoma kisu mwalimu hadi kufa katika shule moja katika mji wa Saint-Jean-de-Luz nchini Ufaransa.

Msemaji wa Serikali ya Ufaransa Olivier Véran amethibitisha shambulio hilo la Jumatano na kusema kuwa mshukiwa alikuwa na umri wa miaka 16.

Polisi walifika shule ya Saint-Thomas d’Aquin pamoja na mwendesha mashtaka wa eneo hilo, ambapo mwanafunzi huyo alikamatwa.

Gazeti la Kifaransa la Sud Ouest lilisema mshambuliaji huyo aliingia darasani wakati mwalimu alipokuwa akifundisha Kihispania na kumshambulia.

Mwalimu huyo alikuwa na umri wa miaka 50 na alikufa kwa mshtuko wa moyo baada ya huduma ya dharura kufika shuleni, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

Kituo cha Televisheni cha Ufaransa BFM kilisema mshambuliaji alifunga mlango wa darasa na kumchoma kisu mwalimu kifuani.

Mwendesha mashtaka wa eneo hilo Jerome Bourrier alisema kuwa uchunguzi umefunguliwa na Polisi wa eneo hilo kwa mauaji na mshukiwa yuko kizuizini.

Waziri wa Elimu wa Ufaransa Pap Ndiaye amelitaja shambulio hilo kuwa “janga lenye uzito wa kupindukia” na kutuma salamu zake rambirambi.

By Jamhuri