Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA),Dk.Stephan Ngailo amesema wanatarajia kuongeza upatikanaji wa mbolea kutoka tani 586,604 mwaka 2019/2020 hadi tani 800,000 Mwaka 2020/2025 ili kuongeza uzalishaji wenye tija.

Aidha mpaka kufikia Juni 30,2023 upatikanaji wa mbolea ulikuwa tani 1,115,841 ambapo lengo limefikiwa na kuvuka kabla ya miaka miwili ya ilani kukamilishwa kwa asilimia 139.48.

Hayo aliyasema Leo Julai 17,2023 jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa katika Ilani ya CCM ukurasa wa 39 inaeleza na kuelekeza kuwa itaongeza usambaji wa pembejeo za kilimo kwa gharama nafuu ikiwa ni pamoja na mbolea.

Alisema kuwa ilani inaelekeza kuimarisha ukaguzi wa mbolea, mbegu na viatilifu kwa kuanzisha na kuimarisha ofisi za Kanda nchini ili, Mamlaka imeanzisha Kanda Tano ambazo ni

“Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na Kanda Mashariki lakini pia kujenga maabara ya Kitaifa ya kudhibiti ubora wa mbolea; ujenzi umekamilika na shughuli za uchambuzi wa mbolea zimeanza Julai, 2023,”alisema.

Pamoja na hayo inahamasisha ujenzi wa viwanda vipya vya kuchanganya mbolea na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha mbolea, chokaa kwa ajili ya kilimo na viuatilifu ifikapo 2025.

“Viwanda vya mbolea kumi na saba vinazalisha mbolea , Viwili ni vikubwa na kumi na tano ni vya kati na vidogo”amesema.

Akizungumzia mpango wa maendeleo wa miaka mitano awamu ya tatu alisema kuwa ni pamoja na kuendelea kujiimarisha katika masuala ya ushindani katika viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu,kufungua fursa za kiuchumi, kujenga uchumi wa Viwanda, kuimarisha ushindani wa ndani na wa kikanda na masoko ya kimataifa.

Aidha katika kujenga uchumi wa viwanda kilimo kinachangia asilimia 65 ya malighafi za viwandani.

“Mamlaka itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa Viwanda vya kuzalisha mbolea nchini na kuwa kitovu cha mbolea katika ukanda huu wa Africa Mashariki na SADC,”amesema.

Amesema mpango na bajeti wa Mamlaka katika mwaka 2023/2024 Ruzuku ya Mbolea kuwa Serikali imetenga bajeti ya Shilingi 150 Billioni kwa ajili ya ruzuku ya Mbolea.

“Mamlaka itaendelea kuratibu na kusimamia utoaji wa ruzuku kwa wakulima, Mpango wa Maendeleo wa Kilimo wa II (ASDPII),Kuimarisha tija na faida katika kilimo kwa kuboresha upatikanaji na ufikiwaji wa pembejeo za kilimo,”amesisitiza.

Pamoja na hayo amesema kutokana na kupanda kwa bei za mbolea katika soko la dunia, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima kwa lengo la Kupunguza gharama ya mbolea, Kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, Kuimarisha usalama wa chakula, Kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda vya ndani

“Mbolea za kupandia na kukuzia zinahusika katika mpango wa ruzuku kulingana na mahitaji, Mfumo wa kidijitali (Digital Platform) unatumika kuratibu usajili wa wanufaika, usambazaji, mauzo na malipo ya fedha za ruzuku” amesema.

By Jamhuri