Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Katika kuhakikisha inakuza ubunifu kwa kampuni changa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini, Tume ya Tehama (ICTC) imefanikisha safari ya wabunifu saba kwenda Algiers, Algeria kushiriki katika kongamano la kimataifa la Tehama barani Afrika litakaloshirikisha zaidi ya mataifa 50 kuanzia leo.

Kwa kushiriki katika kongamano hilo la siku tatu, wabunifu hao wa Kitanzania watapata fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutangaza kazi zao, kukutana na wataalamu wengine wa Tehama kutoka sehemu mbalimbali duniani ambako wanatarajiwa kujifunza kuelekea katika ukuaji wao kisekta.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dkt. Nkundwe Mwasaga, akizungumza jana jijini Dar es Salaam, alisema kwa Tume na taifa kwa ujumla, kongamano na maonesho hayo ni faida kubwa kwa nchi kwani vitasaidia kukuza na kuvutia uwekezaji wa Tehama nchini.

“Hiyo ni hatua kubwa kwetu kama Tume ya Tehama lakini pia kwa nchi. Haya ni matunda ya uratibu wa programu ya kukuza kampuni changa za TEHAMA (ICT Startups) ili kuwezesha bidhaa za TEHAMA kuingia katika soko na kuchangia katika kukuza uchumi na kutengeneza ajira kwa vijana. Tume imewezesha kampuni changa kadhaa kuanza kutoa huduma,” alisema.

Kwa mujibu wa Dkt. Mwasaga, ushiriki katika kongamano hilo kubwa Afrika umewezeshwa na ICTC. Ameishukuru Serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa nguvu sekta ya tehama katika mpango wa kujenga uchumi wa kidigitali, kwani umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha safari ya wabunifu hao.

Katika kongamano hilo linalotarajiwa kuhudhuriwa na wabunifu 500, watazamaji zaidi ya 10,000, wawekezaji 200, wabobezi katika sekta ya tehama wapatao 100, kampuni za Tanzania zinazotarajiwa kushiriki ni Ngasmake (Lipa kwa Ngasmake (Lipa kwa Uhakika), Niajiri, Neuro-Sarufi AI, Simplitech, Mipango App, Scancode na Settlo.

Benki ya CRDB iliyoingia makubaliano na Tume ya Tehama kuendeleza Wabunifu wa Kampuni ndogondogo za TEHAMA kupitia programu ya Imbeju, pia ni sehemu ya washiriki.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Tume ya Tehama ambaye yuko Algeria na wabunifu hao, Jasson Ndanguzi aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, akizungumzia manufaa ya ICTC kushiriki katika kongamano na maonesho hayo, alisema ni pamoja na kusaidia kuvutia na kuongeza fursa za uwekezaji mitaji katika kampuni bunifu za TEHAMA nchini.

“Pia kuna fursa ya kuongeza ujuzi wa programu za uanzishwaji wa vituo vya bunifu za TEHAMA nchini kwa kujifunza kutoka nchi zingine zinazoshiriki kongamano hilo, kupata washirika wa kuendesha programu za ubunifu wa kidijitali na kukuza soko la bidhaa za TEHAMA zinazotokana na bunifu za TEHAMA ili kukuza pato la taifa lakini pia kutangaza nafasi ya Tanzania katika uwanda wa masuala ya bunifu za kidijitali.

“Na zaidi ya yote, ni fursa ya kuzitangaza kampuni changa zenye bunifu za TEHAMA ili ziweze kupata mitaji au/na washirika wa biashara nje ya mipaka ya Tanzania kama moja ya mkakati ya kukuza matumizi ya bunifu za TEHAMA nje ya nchi na hatimaye kuongeza pato la fedha za kigeni,” alisema Ndanguzi.

Ukuzaji na kuvutia uwekezaji ni moja ya majukumu ya Tume ya Tehama inayotekeleza Sera ya Taifa ya Tehama pamoja na sera nyingine zinazohusiana na kuendeleza matumizi ya tehama, lengo likiwa kutengeneza ajira na kuchangia katika shughuli za kiuchumi na kijamii, huku ikiimarisha uratibu wa shughuli za Tehama ili kuongeza mchango wa sekta husika katika uchumi wa taifa.

Tume, kwa sasa inaelekeza nguvu katika kuanzisha vituo vya ubunifu wa Tehama kote nchini, ikianza na mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma, Tanga, Mbeya, Lindi na Zanzibar, lengo likiwa kusogeza huduma karibu na wananchi, hasa ikizingatiwa kumekuwa na ongezeko la uhitaji wa matumizi ya Teknolojia kwenye uchumi wa Tanzania.

By Jamhuri