Baada ya Lowassa kufika Ikulu kumtembelea Rais Magufuli, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amezungumzia kitendo kilichotokea kwa Mh. Lowasa kwenda Ikulu bila makubaliano ya chama(CHADEMA)

Nanukuu kutoka kwenye page yake ya Instagram
“Naomba na mimi niseme kwa uchache kuhusu suala la Mheshimiwa Lowasa. Baada ya Mwenyekiti kuzungumzia jambo hili, inaelekea kuwa wazi kwamba Mheshimiwa Lowassa hakumshirikisha Mwenyekiti kabla ya kukubali au kuamua kwenda Ikulu kukutana na Rais Magufuli.
Na juzi tu wakubwa wetu hawa wawili walikuwa pamoja hospitalini kumsalimia Mzee Ngombale Mwiru.
Je, inawezekana Mheshimiwa Lowassa hakuwa anajua tayari kwamba ana appointment Ikulu?
Kama alikuwa anajua, kutokumshirikisha Mwenyekiti wake kuna tafsiri gani hasa? Katika mazingira ya sasa ya Tanzania ya Magufuli, uamuzi wowote wa kufanya nae mazungumzo, hata kwa nia njema yoyote ile, bila kushauriana au kuwashirikisha viongozi wa juu wa chama, ni uamuzi usio sahihi na mgumu kukubalika.

Vile vile, kauli za aina ambayo tumeisikia kutoka kwa Mheshimiwa Lowassa, zina athari kubwa kisiasa sio tu zinachanganya wanachama na wafuasi wetu, lakini pia zinawapa mtaji wa kisiasa maadui zetu. .
Kuanzia sasa tutegemee sana kuwasikia CCM wakishangilia ‘busara’ za Mheshimiwa Lowassa.

Masuala ya ukiukwaji haki za binadamu, uvunjwaji wa Katiba na mengine mengi sasa yatajibiwa kwa namna moja.

Lowassa amemkubali Magufuli nyie wengine mnapiga kelele za nini. Huu ni mtaji wa bure kwa Magufuli. Ukweli, ambao umesemwa sana humu, ni kwamba amefeli karibu katika kila jambo. Hata hiyo reli anayosifiwa nayo na Lowassa bado ni ndoto tu: nani ajuaye itajengwa kwa hela za nani??? .
Za Wachina kama tulivyoambiwa mwanzoni; au za Waturuki kama tulivyoambiwa baadae; au za Afrika Kusini kama alivyosema mwenyewe anaenda kumwomba Zuma??? .
Kama chama hatujawahi kukataa mazungumzo na Rais au kiongozi mwingine yeyote wa serikali.

Na hatukatai kuzungumza na Magufuli kuhusu matatizo mengi na makubwa yanayoikabili nchi yetu. .
Lakini ni muhimu na lazima viongozi wakuu wa chama washirikishane na washauriane kabla ya mazungumzo hayo. .
Na baada ya mazungumzo, ni lazima viongozi wakubaliane juu ya kauli za kutoa hadharani kwa umma ili wote tuwe kwenye ukurasa mmoja. .
Katika mazingira ya sasa, ambako viongozi na wanachama wetu wanashambuliwa hadharani kwa mapanga na hata kwa risasi, kumsifia Rais ni kumuunga mkono yeye na matendo yake. .
Katika mazingira ya kesi nyingi za kutunga dhidi yetu, ‘kazi nzuri’ inayofanywa na Magufuli ina maana gani hasa, kama sio kuhalalisha ukandamizaji tunaofanyiwa. .
Katika mazingira ambapo hata jumuiya ya kimataifa imeanza kuhoji mwenendo wa Rais Magufuli, kutoa kauli kwamba ‘anafanya kazi nzuri’ ni ‘kumtupia taulo’ la propaganda litakalomfichia madhambi mengi aliyowafanyia Watanzania katika miaka hii miwili. .
Kwa vyovyote vile, kitendo cha Mheshimiwa Lowassa sio cha kunyamaziwa au kuhalalishwa kwa hoja nyepesi nyepesi”.

By Jamhuri