Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Serikali imeviasa vyama vya siasa kuendelea kuimarisha mazungumzo, ushirikiano na umoja wa kitaifa wakati Tanzania ikijiandaa kuanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mwezi Julai mwaka huu.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, wakati akifungua warsha ya wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa mjini Morogoro tarehe 17 Juni 2026. Warsha hiyo yenye lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu jukumu jipya la Mahusiano ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa siasa.
Kwenye hotuba yake Waziri Sangu amesema vyama vya siasa ni wadau muhimu katika kukuza amani, umoja na ustawi wa jamii. Ameongeza kuwa, utayari wao wa kushirikiana na Serikali ni muhimu katika kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo vyama vya siasa vyenyewe.
Amewapongeza na kuwaasa viongozi wa kisiasa kuendelea kuwa mabalozi wa amani na kutokubali kutumiwa na watu wachache wenye maslahi binafsi wanaoweza kuligawa taifa au kuhatarisha utulivu na amani ya nchi.
“Leo tunapozungumzia mahusiano kati ya Serikali na vyama vya siasa, niwahakikishie kuwa dhana hii inaendelea kutekelezwa kupitia falsafa maarufu ya 4R iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kujenga taifa lenye amani na umoja,” alisisitiza Waziri Sangu.
Amesema falsafa hiyo ya Rais Samia ya 4R, ambayo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Ujenzi Upya, inaendelea kuongoza jitihada za Serikali katika kukuza mazungumzo, kuimarisha kuaminiana na kujenga taifa lenye umoja kupitia ushirikishwaji mpana.
Waziri Sangu amelipongeza Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuendelea kushirikiana na Serikali, ikiwemo kutoa ushauri katika masuala mbalimbali ya kitaifa. Amesema ushirikiano huo ni muhimu wakati nchi ikielekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inahitaji mshikamano na malengo ya pamoja bila kujali tofauti za kisiasa.
Akiunga mkono ujumbe huo, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Mhe. Juma Ali Khatibu, amesema vyama vya siasa vina nafasi kubwa katika jamii ya Watanzania na vinaweza kusaidia kuimarisha mahusiano, amani na maelewano ndani ya jamii.
Khatibu ameongeza kuwa Baraza hilo linatambua dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza siasa za ushirikishwaji. Ametolea mfano uteuzi wa mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo, Dkt. Eveline Wilbard Munisi kutoka NCCR-Mageuzi, kuwa Mbunge na Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano. Amesema uteuzi huo unaonesha kuaminiana, ushirikishwaji na ushirikiano katika siasa za ushindani nchini.




Mkurugenzi wa Idara ya Mahusiano, Bw. Rasheed Maftah, akiwasilisha mada kuhusu dhana ya mahusiano wakati wa Warsha ya Viongozi na Wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa, iliyofanyika katika Ukumbi wa Nashera, Mkoa wa Morogoro, leo tarehe 17 Juni 2026.

