Unyama!Mume amuua mke na kumtumbukiza kisimani

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Tabora

JESHI la Polisi Mkoani Tabora linamshikilia Ali Idd Mkonongo, mkazi wa Kijiji cha Inala kata ya Ndevelwa, katika Halmashauri ya Manispaa Tabora, kwa tuhuma za kumuua mke wake, aliyetambulika kwa jina la Mariam Yusuph, kwa kumpiga na kitu kizito kichwani wakati akiwa amelala kisha kutumbukiza mwili kisimani kwa lengo la kupoteza ushahidi.

Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ACP Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo na kubainisha kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Septemba 18, mwaka huu majira ya saa sita usiku katika Kijiji hicho .

Amesema mtuhumiwa alienda kufanya tukio hilo baada ya kutoka kwa mganga wa kienyeji ambako alienda kupigisha ramli ili amwone mchawi wake kwenye ndoto.

Kamanda amesema baada ya kutoka kwa mganga mwanaume huyo alidai kumwona kwenye ndoto mkewe huyo hivyo akaamua kutekeleza kile alichokusudia.

Amebainisha kuwa wanamshikilia mtuhumiwa huyo na wanaendelea na uchunguzi dhidi ya kitendo hicho kabla ya kumfikisha mahakamani.

Amesema licha ya kumtia mbaroni bado wanaendelea kuwasaka washirika wenzake akiwemo mganga huyo wa kienyeji.

Aidha Kamanda Abwao amesema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika taratibu za uchunguzi.