Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya ufundi stadi(VETA)kwa kushirikiana na Shirika la ushirikiano wa kimataifa la Ujerumani (GIZ) Kupitia programu ya kukuza Ajira na ujuzi kwa Maendeleo Afrika (E4D), imeandaa kongamano la Ajira litakakofanyika Agosti 24,2023 jijini Dodoma.

Mwakilishi wa Mkurungezi Mkuu wa VETA Abdallah Ngodu Amesema hayo leo Agosti 22,2023 jijini hapa Wakati akitoa taarifa ya Kongamano la ujuzi na Ajira Kupitia Programu ya kukuza Ajira na ujuzi kwa Maendeleo Afrika E4D.

Amesema, Kongamano hilo litakuwa na maonesho ambayo yamelenga Kujenga uelewa wa fursa za ufundi stadi zilizopo kwenye Mradi ,kukuza uwezo wa kujiajiri na kuajirika pamoja na kushirikishana taarifa za soko la ajira.

“Wananchi watapata fursa ya kujionea shughuli zinazofanywa na wahitimu na wanufaika wa Mradi wa E4DT pamoja na kupata taarifa ya fursa ya Mafunzo ya ufundi stadi kwenye vyuo vya VETA nchini,”amesema

Ngodu amesema utekelezaji wa Mradi huo unahusisha ushiriki wa viwanda ambapo mpaka Sasa Jumla ya viwanda 20 vimethibitisha kushiriki na kuonesha huduma na bidhaa zao kupitia kongamano hilo.

“Tanzania ni miononi mwa nchi Sita za Afrika zinazotekeleza Mradi wa stadi za Ajira kwa Maendeleo Afrika (E4D) inayofadhiliwa na wizara ya shirikisho la Ujerumani (BMZ)na shirika la ushirikiano wa Maendeleo la Korea(KOICA);

Mradi huu wa E4D ulianza kutekelezwa Mei 2022 ukilenga kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana 4000 nchini, Katika fani za ufundi bomba wa majumbani, viwandani, uchomeleaji vyuma viwandani na ufundi wa mekatroniki, “amesema

Pamoja na hayo ameeleza kuwa hadi sasa Jumla ya vijana 3,258 wamenufaika na mafunzo Katika vyuo vya VETA vya Dodoma, Manyara, Lindi, Singida, Mikumi, Gorowa na Dakawa Katika awamu nne .

Kwa Upande wake Mkuu wa Chuo Cha VETA Dodoma Stanslaus Ntabara amesema Hadi kufikia Agosti 19,2023 Jumla ya wanafunzi 1806 wa Mkoa wa Dodoma wamehitimu Mafunzo hayo .

“Udahili wa awamu ya tano ukiendelea na mafunzo hayo yametolewa kwa wiki nane vyuoni na wiki nane mahali pa kazi, matarajio , tunatarajia kuwa nguvukazi yenye ujuzi kutokana na mradi wa E4D itatumika Katika kukuza Ajira kwenye Miradi ya kimkakati ya uwekezaji Kama vile bomba la mafuta , bwawa la Nyerere la uzalishaji wa Nishati ya Umeme na treni ya mwendo kasi , “amesisitiza

Naye mwakilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya ushauri elekezi (GOPA) Leah Dotto ameipongeza VETA katika ushiriki wake Katika kutoa mafunzo yaliyoendelea na yaliyowahi kufanyika na kuelekeza kwamba jamii itanufaika na kuwa na vijana wenye Ajira na wanaoweza kuajirika Katika uwekezaji wa viwanda.

“Niwaombe vijana muwe tayari kwenye uwekezaji kwani Kupitia Mafunzo haya vijana wataweza kupata Ajira kwenye Miradi ya kimkakati na kuondokana na tatizo la ajira kwa vijana waliokosa Ajira,”amesema

By Jamhuri