Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar

Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mussa Azan Zungu ambaye pia ni mbunge wa Ilala amewaasa Watanzania kushiriki kikamilifu Sensa ili kutimiza lengo la Serikali kupata takwimu za msingi za watu na hali za makazi ambazo zitasaidia kutunga sera, kupanga na kufuatilia mipango ya maendeleo.

Baadhi ya wananchi wakisikiliza elimu ya Sensa katika viwanja vya Mchikichini leo

Sensa ya watu na makazi inatarajia kufanyika Agosti 23,mwaka 2022 siku iliyotangazwa Rais waSamia Suluhu Hassan kuwa ni siku ya mapumnziko.

Akizungumza leo Agosti 21, 2022 katika viwanja vya Kata ya CCM Mchikichini katika uelimishaji wa sensa kwa wanachama na wananchi wa kata hiyo, Zungu alisema kuwa Sensa ina umuhimu mkubwa wa taifa.

“Tunapaswa kushiriki Sensa kikamilifu kwani litaisaidia taifa kupata takwimu za msingi zitakazotumika kuleta maendeleo nchini,” amesema.

Naye katibu wa Kata ya Mchikichini Hellen Madanganya amesema kuwa
Sensa ya watu na makazi ni moja ya zoezi linalokusanya taarifa za kila mtu aliyelala ndani ya mipaka ya nchi usiku wa kuamkia siku ya Sensa.

Katibu huyo amesema kuwa sensa ya Mwaka 2022 kama zilivyo Sensa zilizopita,itahusisha Makarani wa Sensa ambao watatembelea kaya zote nchini na kufanya Mahojiano ya ana kwa ana baina ya Karani wa Sensa na Mkuu wa kaya. Ikiwa Mkuu wa kaya hatakuwepo, karani wa Sensa atafanya Mahojiano na mtu mzima yeyote katika kaya ambae ana taarifa za kutosha kuhusu kaya na wanakaya wenzake waliolala katika kaya husika usiku wa kuamkia siku ya Sensa.

Madanganya amesema kuwa lengo la Sensa ya watu na makazi ni kupata taarifa sahihi za Kidemografia, Kijamii, Kiuchumi na hali mazingira kwa lengo la kupata takwimu sahihi zitakazoiwezesha serikali na wadau wengine kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta mbalimbali za elimu, afya, hali ya ajira ,miundombinu kama barabara,nishati na maji safi.

Kwa msingi huo, Sensa ni zoezi muhimu ambalo kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kushiriki na kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha inakuwa ya mafanikio makubwa.

“Hii itasaidia serikali kutimiza wajibu wake kwa wananchi kulingana na idadi ya watu ya eneo husika ikiwa kama msingi mkubwa wa ugawaji ya keki ya Taifa kwa kila eneo la utawala hapa nchini” amesema Madanganya.

Katibu wa Kata ya Mchikichi Hellen Madanganya
Mwenyekiti wa Kata ya Mchikichini Yakoub Kabyemela na katibu Hellen Madanganya

By Jamhuri