Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
SERIKALI imeanza uchunguzi maalumu kubaini upungufu katika viwanja vyote vya ndege nchini na kuzifanyia kazi ikiwemo mifumo, utendaji na miundombinu ili kuboresha sehemu husika.
Lengo ni kurahisisha uingiaji na utokaji wa wageni ikiwamo watalii wanaokuja nchini . Inalenga pia kudhibiti uhalifu unaotokea katika viwanja vya ndege ikiwamo utoroshaji wa vito vya thamani, mnyororo wa upitishaji na uingiaji wa dawa za kulevya na wageni bila kufuata sheria na taratibu za kiuhamiaji.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Kamati ilitembelea na kukagua mifumo ya uhamiaji mtandao katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Ujenzi wa Chuo cha Uhamiaji Kitogani na Ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi Mazizini.
“Mbali ya kazi nzuri ambazo zinafanywa na Uhamiaji, lakini kuna maeneo tunataka kupeleka nguvu zaidi hasa maeneo ambayo kwanza ni sura ya nchi, malango makuu ya kuingilia kama hapa tulipo katika maeneo ya viwanja vya ndege,”alisema.
Alisema, “mtu akija Tanzania sura ya nchi inamuonesha anapopokewa katika viwanja vya ndege, haipendezi mgeni akija hapa nchini apange mstari mrefu, mara viyoyozi havifanyi kazi ndiyo maana serikali kuna uchunguzi maalumu tunafanya ili kuweza kubaini upungufu huo na kufanyia kazi katika viwanja vyote vya ndege nchini.”
Akizungumza katika ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje,Ulinzi na Usalama, Vicent Mbogo alisema ni muhimu upungufu huo katika viwanja vya ndege ukafanyiwa kazi.
Alisifu juhudi za serikali zote mbili katika kuiletea Zanzibar maendeleo ambayo alisema Zanzibar ni nchi ya utalii hivyo ni vyema huduma katika malango yake yakaboreshwa.
Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ali Hassan alitaja miradi ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2023/2024 iliyokamilika ikiwamo ujenzi wa ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkoa wa Kusini Pemba ukarabati wa ofisi kuu ya Uhamiaji Zanzibar.
Pia ukarabati wa nyumba ya makazi ya askari Ndugu Kitu Chakechake, Pemba na ukarabati wa nyumba mbili za makazi ya askari Mtemani Wete na Pemba imekamilika kwa asilimia 100 huku gharama yake ikiwa ni Sh bilioni 1.9.