Baadhi ya wagonjwa wanahaha mjini hapa baada ya Serikali kupitia Idara ya Afya Mkoa wa Geita, kufunga Kituo cha Afya cha Msufini kilichopo Mtaa wa Msalala, Kata ya Kalangalala wilayani Geita.

Uongozi wa kituo hicho umeagizwa kuomba upya usajili wa kituo hicho, mbali ya kuwa usajili ulifuata miongozo yote ya kuendesha zahanati binafsi, ikiwa ni pamoja na kulipa ada ya kila mwaka kwa kiwango kinachopendekezwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Uamuzi huo uliolalamikiwa na mamia ya wananchi wa mji wa Geita waliokuwa wakipatiwa huduma za uhakika kwenye kituo hicho, huku wengine wakihusisha tukio hilo na mazingira ya rushwa, umefikiwa na Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) wa Geita, Dk. Joseph Kisala.

Mmiliki wa zahanati hiyo ambaye pia anamiliki Chuo cha Ukunga na Uuguzi cha GMLTC, Dk. Paul Alphonce,  amethibitisha kufungwa kwa zahanati hiyo kunakochochewa na Muuguzi wa Wilaya (DNO) ya Geita, Ifigenia Chagula, anayejiapiza kumkomesha mmiliki wa hospitali hiyo aking’ang’ania apewe hisa za umiliki.

Mvutano wa wadau hao wa tiba ulifikia hatua ya kuingiliwa kati na Mbunge wa Busanda anayemaliza muda wake, Lolensia Bukwimba.

JAMHURI imebahatika kupata nakala ya nyaraka iliyofunga zahanati hiyo yenye Kumb. Na BA/162/279/01/43 ya Agosti 3, 2015 yenye kichwa cha habari, ‘Ilani ya Kufunga Huduma za Kituo Binafsi cha Huduma za Afya Kinachoitwa Msufini.’

Katika barua hiyo iliyosainiwa na RMO, Dk. Kisala, inasema. “Kutokana na ukaguzi uliofanywa na wakaguzi kutoka Mkuu wa Mkoa wa Geita, Agosti 3, 2015 ilionekana unaendesha Zahanati ya Msufini kinyume cha Sheria ya Hospitali Binafsi ya mwaka 1977, iliyorekebishwa mwaka 1991, kifungu Na. 5(1) Na. 9(1) na Na 6 na mwongozo wa kuanzisha na kuendesha kituo cha huduma za afya kwa kuzingatia yafuatayo:

“Mosi, kutokuwa na usajili wa zahanati hiyo, na pili, mikataba ya ajira ya watumishi haipo, hivyo unatakiwa kufunga moja kwa moja kwa muda kurekebisha mara moja kasoro zilizoainishwa hapo juu, kuanzia tarehe ya kupata ilani hii hadi hapo utakapokamilisha marekebisho ya kasoro zilizoainishwa na kutoa taarifa kwa Mganga Mkuu wa Wilaya, na nakala Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, ili ukaguzi ufanyike tena kutathmini urekebishaji wa kasoro hizo. Umepewa muda kufanya marekebisho hayo.

“Unatakiwa kufanya marekebisho ya kasoro zilizoainishwa kwa kufanya yafuatayo: Mosi, kuomba usajili upya wa kituo husika kwa mamlaka husika na kufuata miongozo yote ya kuendesha zahanati binafsi,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ambayo nakala yake imetumwa kwa Mganga wa Wilaya, Mtendaji wa Kata, Kamanda wa Polisi Mkoa, na Mkuu wa Kituo cha Polisi Geita.

Baada ya kujiridhisha kuwa zahanati hiyo imesajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi na inafuata miongozo ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, JAMHURI ilimtafuta Dk. Kisala kwa njia ya simu ili kujua iwapo kuna ajenda ya siri iliyosababisha zahanati hiyo kufungwa; yakiwamo mazingira ya rushwa kama wananchi wanavyodai.

Hata hivyo, Dk. Kisala alikana kuifunga zahanati hiyo, lakini alipobanwa kwa maswali alikiri huku akitaja sababu zilizoainishwa kwenye barua yake, alipotakiwa kueleza mamlaka ya ofisi yake kwenye usajili wa zahanati binafsi na kudai wahusika ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

“Sitambui tukio hilo labda nifuatilie ili nibaini nani aliyefunga. Oooh! nimekumbuka, Msufini nimeifunga kwa sababu haijasajiliwa, usajili uliopo ni feki, ni mambo mawili ambayo nimeelekeza yafanyike kuomba upya usajili na pia mikataba ya watumishi. Wanaosema natumiwa na wamiliki wa hospitali binafsi hilo ndiyo nalisikia kwako, mimi siwezi kutumika wala kuomba rushwa,” anasema Dk. Kisala.

Wakati Dk. Kisala akibainisha upungufu, JAMHURI imeona mikataba ya wafanyakazi pamoja na cheti cha usajili wa zahanati hiyo, kilichotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Machi 10, 2011 baada ya mmiliki wake kukamilisha taratibu zote za usajili wa kituo hicho ikiwamo wizara kujiridhisha na ripoti ya wakaguzi waliofika eneo ilipo zahanati hiyo na kufanya ukaguzi uliosababisha wizara kutoa kibali cha kuanzishwa kwa zahanati hiyo.

JAMHURI pia imebahatika kuona ripoti ya wakaguzi kutoka Idara ya Afya kwenda wizarani ya Machi 31, 2008 yenye Kumb. Na. GDC/DR/VOL 1/8 ikiwa na kichwa cha habari, “Taarifa ya Ukaguzi wa Zahanati Mpya ya Paul eneo la Msufini,” iliyoandikwa Aprili 2, 2008 ikiwa ni siku mbili baada ya ukaguzi huo kufanyika.

Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo imebainisha masuala kadha wa kadha waliyobaini ikiwa ni pamoja na kuangalia iwapo mmiliki wa zahanati hiyo amekidhi vigezo vya kufungua zahanati kwenye eneo husika, kwa kutoa huduma za wagonjwa wa nje, maabara pamoja na huduma za uzazi na mwisho wa ripoti hiyo wakaguzi ambao ni Dk. C. Kabuche (M.O.I/C), M.L. Lupandisha (DHO), R. Msuya (Mfamasia) na R. Binamungu (DNO) – wote kutoka Geita.

Katika ripoti yao wamesema: “Wakaguzi wanapendekeza zahanati hii ipewe kibali kulingana na mwongozo wa wizara juu ya uanzishaji wa zahanati, idara ipitishe maombi ya kibali cha zahanati husika ili ipewe kibali na mamlaka husika,” ilihitimisha barua hiyo.

Kutokana na ukaguzi huo, Mei 15, 2015 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilikubali maombi hayo kwa barua Kumb. Na. HC 213/453/01A/177 iliyokuwa na kichwa cha habari, “Ombi la Kufungua na Kuendesha Msufini Dispensary Geita,” ambako pamoja na mambo mengine, sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Dk. P. L. Sawa, Msajili wa Hospitali Binafsi, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara.

“Napenda kukutaarifu kuwa kikao cha Bodi ya Ushauri ya Hospitali Binafsi cha Mei 4 na 5, 2009 kimelijadili ombi lako la kufungua na kuendesha kituo cha kutolea huduma za afya kitakachojulikana kama Msufini Dispensary, kwenye eneo la Kalangalala, katika Wilaya ya Geita, Mkoa wa Mwanza limekubaliwa kwa kufuata masharti yafuatayo:

“Mosi, utafuata na kuzingatia miongozo ya vituo vya kutolea huduma za afya na miongozo mingine itakayotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; pili, kulipa ada ya mwanzo Sh. 80,000 na ada ya kila mwaka kwa kiwango kitakachopendekezwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, namba ya usajili wa kituo chako ni 196205, cheti cha usajili wa zahanati yako kinatayarishwa, kikiwa tayari utapewa, tafadhari fuatilia,” ilisomeka barua hiyo iliyosainiwa na Dk. P. L. Sawa, Msajili wa Hospitali Binafsi kwa niaba ya Katibu Mkuu, nakala yake kupewa Mganga Mkuu wa Mkoa na Wilaya ya Geita.

Kwa upande wake, Dk. Paul ameshangazwa na hatua hiyo iliyochukuliwa na Dk. Kisala dhidi ya zahanati yake, akidai, “Wamepania kunifilisi. Sitakubali matakwa ya baadhi ya vigogo wa idara hiyo hususani kwenye Wilaya ya Geita,” na kuahidi kupambana kufa na kupona ili kuhakikisha anayashinda majaribu yanayomtokea na kusonga mbele kwa kuwa shughuli zake zipo kihalali.

Alidai kuwa pamoja na zahanati yake kusajiliwa mwaka 2011 na kupewa namba 19605, na kuruhusiwa kufanya kazi zake kwenye eneo la Kalangalala katika Wilaya ya Geita mkoani Mwanza, kabla ya kuwa Mkoa wa Geita, ameshangaa kufungwa huku akilihusisha tukio hilo na vitisho ambavyo amekuwa akivipata kutoka kwa baadhi ya vigogo wa idara hiyo akiwamo DNO Chagula, aliyegoma kumpa hisa kwenye Chuo chake cha Ukunga na Uuguzi.

“Hili tukio si la bahati mbaya, huyu mganga amefanya hivyo kwa makusudi na ninajua ni kina nani wanaomjaza maneno ya uzushi, maana haiwezekani ninafungiwa kituo kwa sababu za kutunga kama hizi, eeti usajili wa kituo changu umepewa dosari kwamba eneo kilipo si kilipotakiwa kuwa,” alisema na kuongeza:

“Hapa kilipo panaitwa Msufini na ndiyo jina la zahanati yangu, jina la kata halijabadilika na hata lingebadilika si kosa langu kwani mabadiliko ya mtaa yamefanywa na Serikali kwa mujibu wa sheria maana wakati tunasajili tulikuwa chini ya Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Geita, halafu naambiwa niombe upya usajili huu unaitwa feki, niwe na usajili feki nilipie mapato Serikalini?’’ Alihoji Dk. Paul.

 Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na kuendesha kazi zake kwa kufuata sheria za nchi, amekuwa akikumbana na changamoto nyingi kutoka kwa baadhi ya vigogo wa idara hiyo, na wengine wamediriki kumuomba rushwa, jambo ambalo alikwishaapa kutolitekeleza kwa kuwa ni kosa kisheria.

Kabla ya kituo kufungwa, Julai 21, 2015 asubuhi, alitembelewa na wageni watatu akiwamo David Mshandete (Mfamasia wa Mkoa), Simon Ndalilo (Mjumbe wa Kamati ya Idara ya Afya) pamoja na Dk. Nyang’ombe, daktari wa meno mkoani Geita.

By Jamhuri