Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

KATIKA jitihada za kuandaa wahitimu wanaoendana na soko la ajira duniani, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kimeanzisha ushirikiano na kampuni ya RSM Eastern Africa ili kuwajengea uwezo wanafunzi wake katika eneo la uhasibu na elimu ya fedha.

Kupitia ushirikiano huo RSM itatoa mafunzo kwa wanafunzi wa chuo hicho katika maeneo matatatu ambayo ni ukaguzi wa hesabu, za fedha, elimu ya kodi, elimu ya kutoa ushauri wa kitaalamu.

Akifungua mafunzo hayo jana chuoni hapo, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Emmanuel Munishi, alisema mnbali na CBE, mafunzo hayo yatatolewa pia kwa wanafunzi wa vyuo vingine.

“CBE itakuwa ni kituo tu au Hub ya mafunzo hayo kwa taasisi zote za elimu ya juu Tanzania na kwenye program hii tunatarajia kuwanufaisha wanafunzi 3,000 wanaosomea Shahada za Uhasibu, uhasibu na fedha pamoja na taaluma ya benki na fedha,”amesema.

Aidha, amesema mafunzo hayo ambayo yataendeshwa na maafisa waandamizi kutoka RSM Eastern Africa wenye uzoefu wa kimataifa yatasaidia ajenda ya maendeleo ya kimataifa.

Aidha, amesema mafunzo hayo yatasaidia kwenye kufikia lengo la nne la maendeleo endelevu la Umoja wa Mataifa (UN Sustainable Goals) kuhusu elimu bora na hasa elimu ya ufundi na elimu ya fedha ambayo inatolewa na chuo cha CBE.

Amesema mafunzo hayo yatahitimishwa na mashindano a washiriki ambapo washindi watapewa nafasi za masomo kwa vitendo yaani internship na yatasaidia jitihada za chuo kuwaandaa wahitimu kwaajili ya soko la ajira.

Profesa Munishi amesema RSM imekuwa ikifanya kaguzi za hesabu za fedha CBE kwa miaka sita iliyopita na kwa miaka yote hiyo chuo kimekuwa ikipata hati safi na hoja ambazo wamekuwa wakiziibua CBE imekuwa ikizifanyia kazi.

“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa wanafunzi wetu wa CBE na yatatolewa na watu waliobobea kwenye masuala ya ukaguzi hivyo naona wanafunzi mtakaoshiriki kwenye program hii mnabahati kubwa sana na yatasaidia ajenda ya maendeleo ya kimataifa,” amesema Profesa Munishi.

Amesema serikali imefanya maboresho makubwa kwenye mitaala ya elimu na moja ya eneo ambalo imesisitiza ni wanafunzi kusoma kwa vitendo na kwamba elimu ya fedha na biashara ipewe umuhimu wa kipekee.

“Kwa hiyo nyinyi wanafunzi ambao mnasomea uhasibu, fedha, benki na biashara mko katika mazingira mazuri ya kuajiriwa na kujiajiri mtakapomaliza masomo kwa sababu kila kitu duniani kwa sasa kinatoa umuhimu kwa fani hizo,” amesema.

Naye Jovin Bhoke, ambaye ni Meneja wa Kodi wa Kampuni ya RSM, amesema kila mwaka huwa wanaadhimisha siku ya huduma kwa wateja kwa kufanya shughuli mbalimbali za kusaidia jamii.

Amesema katika shughuli hizo huwa wanaangalia ajenda za serikali na zile za kidunia ambapo kwa sasa wameangalia ajenda namba nne ya UN inayojihusisha na utoaji wa elimu bora.

“Tumechagua kuja CBE kwa sababu ni chuo kikongwe kwenye kutoa elimu ya biashara, kodi na elimu ya fedha na tutawashirikisha kile tunachokifanya ili wanafunzi wawe wanasoma kwa kwa vitendo masuala yanayohusu elimu ya fedha,” amesema Jovin.

“Tutawaonyesha wanafunzi kwamba ni kweli kile wanachokisoma kwa nadharia kipo na kinafanyakazi katika ulimwengu wa kibiashara, tutawaonyesha ukaguzi unakuwaje na malengo yake ninini kwa hiyo watapata picha halisi kwamba wanachokisoma darasani kipo kwenye ulimwengu wa taaluma,” amesema.

Amesema RSM ni taasisi ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya ukaguzi wa hesabu za fedha, elimu ya kodi, kutoa ushauri wa kitaalamu na ina uzoefu wa kimataifa wa kufanyakazi katika zaidi ya nchi 120 duniani katika mabara ya Afrika, Asia, Ulaya na Amerika.