Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wanafunzi watatu kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii ni Miongoni mwa wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali Duniani wanaokutana Jijini Nairobi Nchini Kenya kuwania Tuzo ya ‘Hult’.

Wanafunzi hao ni Hellena Sailas, Maria Daudi, na Method Dallu ambao wamechaguliwa kuwania tuzo hiyo kupitia wazo lao la kibishara na kibunifu linalohusu Utengenezaji na uzalishaji wa tofali kwa kutumia taka za plastiki (Recycling of plastic waste into eco-brick).

Tuzo ya Hult Prize ni shindano kubwa zaidi la ujasiriamali wa kijamii kwa wanafunzi duniani, inayoendeshwa kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa na timu za wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani.

Mashindano hayo yanalenga kutatua tatizo la kijamii lenye umuhimu kwa kuanzisha biashara ya kijamii inayoweza kukua na kudumu.

Washindi wa mwisho watawasilisha miradi yao mbele ya jopo la majaji mashuhuri, viongozi wa biashara duniani, viongozi wa mawazo, na watetezi wa mabadiliko ili kushinda dola milioni 1 za Marekani na kuanzisha biashara zao.

Akizungumza na wanafunzi hao ambao wamewasili jana Jijini Nairobi, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dkt. Joyce Nyoni amewapongeza kwa Ubunifu huo na kuwatakia kila⁴ la kheri katika ushiriki wao.