Na Mwandishi wetu Jeshi la Polisi

Wanafunzi toka Chuo cha Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi kutoka Mkoani Mwanza leo wamefika Katika kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia Jijini Arusha kwa ajili ya kujifunza namna ambavyo Kituo hicho kinafanya kazi ya kuwahudumia Watalii na Wageni wanaofika Mkoani humo.

Mkuu wa Kituo hicho, Mrakibu wa Polisi SP Waziri Tenga amebainisha kuwa wanafunzi hao wamepata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kuzingatia usalama wa watalii na wageni pindi wanapowahudumia.

Sambamba na hilo SP Tenga amewasihi Wanafunzi hao kuhakikisha wanakwenda kutoa huduma bora kwa watalii kwa sababu wageni wengi huwa wanatarajia kuona wanapata huduma bora pindi wanapofika Nchini.

Aidha SP Tenga amewaeleza namna ambavyo kituo hicho kimeimarisha mahusiano mazuri kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Sheria, taasisi za Kimataifa lakini pia makampuni yote ya utalii lengo likiwa ni kufikia lengo la Serikali la kuhakikisha watalii na wageni wanakua salama wakati wote.

Mkufunzi toka katika Chuo hicho Bi. Grace Mahendeka amesema lengo la kuwaleta wanafunzi hao katika kituo hicho ni kupata uzoefu wa namna gani kesi mbalimbali za utalii zinashughulikiwa katika kituo hicho lakini pia kuimarisha mahusiano baina ya taaisisi hiyo na Jeshi la Polisi.

Naye Bwana Victor Christian Mwanafunzi toka katika Chuo hicho amesema wamejifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja uhusiano mzuri baina ya Polisi na Makampuni ya Kitalii na taaisisi nyingine ambapo wamepata fursa ya kuona namna ambavyo kesi zinaendeshwa katika Kituo hicho.

Aidha amebainisha kuwa kupitia elimu waliyoipata itawasaidia kuwa na mahusiano mazuri baina yao na taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi lengo likiwa ni kuhakikisha watalii wanakua salama.