Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Handeni

Ikiwa leo ni maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani, wanawake wa Kata ya Kideleko katika Halmashauri ya Mji wa Handeni wametumia nafasi hiyo kupanda miti na kufanya usafi katika bwawa la maji la Kwamaizi katika kata hiyo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Handeni Trunk Main, Yohana Mgaza amesema tangu kuzinduliwa kwake mwaka jana, bwawa la Kwamaizi limekua ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Kata ya Kideleko hasa kinamama ambao wao ndio wana jukumu la kutafuta maji kila siku.

“Hivyo tukaona ni vyema kutumia siku hii kulishafisha na kupanda miti rafiki kuzunguka bwawa hili ili liweze kudumu katika muda uliokusudiwa.

“Bwawa la Kwamaizi katika Halmashauri ya Handeni lilikamilishwa chini ya Ufadhili wa Kampuni ya bia ya Serengeti na kusimamiwa na shirika lisilo la kiserikali la WaterAid ambapo tangu kukamilika kwake mwaka jana linahudumia takribani wananchi 1944,” amesema Mgaza.

Akizungumzia nafasi ya kinamama katika usimamizi wa miradi ya maji na usafi wa mazingira, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Tanzania, Neema Kimaro amesema licha ya mradi huo kulenga huduma ya maji safi kwa wananchi, pia, kuliundwa kikundi maalum cha wanawake 24 waliosajiliwa kwa kazi maalum ya kuwezesha jitihada za kusimamia maswala yote ya uhifadhi wa Mazingira na ulinzi wa miundombinu ya maji ikiwemo usafi katika bwawa.

“Kikundi hiki kitafanya majukumu yake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira – HTM wakiratibiwa na kusimamiwa na Halmashauri ya Mji wa Handeni,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake wanaosimamia mradi huo, Fransisca Mhando amesema: “lengo la hiki kikundi chetu cha kinamama ni kusimamia mauzo ya maji katika hili bwawa ila pia kusimamia matunzo na usafi wa mazingira kwa ujumla katika eneo linalozunguka bwawa,”.

WaterAid ni shirika la kimataifa lenye dira ya kuhakikisha kuwa watu wote ulimwenguni wanapata maji ya uhakika, vyoo bora na huduma za usafi zilizoboreshwa ifikapo mwaka 2030.

WaterAid inafanya kazi katika nchi 28, ambapo nchi 18 zipo barani Afrika. Nchini Tanzania, shirika la Wateraid lilianza kazi 1983 na kufanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya Maji, Vyoo na Usafi binafsi katika zaidi ya mikoa 11.

Aidha shirika limeshirikiana na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo na kuwafikia wananchi zaidi ya milioni nane wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa miji pamoja na vijijini.

By Jamhuri