Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Tabora

Mahakama ya Kuu Kanda ya Tabora imewahukumu watu wanne kunyongwa hadi kufa kwa tuhuma za kuwaua askari wawili wa Jeshi la Polisi wa kituo cha Usoke wilayani Urambo mkoani Tabora.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora aliyekasimiwa na mamlaka hiyo,Ziada Jovinb Katto baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Mahakama hiyo iliwatia hatiani washtakiwa Shedrack Hamis Rushikama, Sylvesta Mussa Kingwendu, Abel Benedict na Ramadhani Kassim Manywele ambao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka mawili ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Amesema kwamba mahakama pasipo shaka yoyote imewatia hatiani washitakiwa hao baada ya kusikiliza ushaidi usiotia mashaka .

Hakimu huyo amesema kuwa kutokana na baadhi ya watu kuamua kujichukulia sheria mkononi hivyo ni fundisho kwa kila moja ambaye anatumia nguvu kupora ama kuua kwa kutoa uhai wa mtu jambo ambalo linapingana na sheria za nchini.

Awali upande wa mashitaka ukiongozwa na Mawakili Meroto Ukongoji na Tunosye Luketa uliiambia mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo mnamo Aprili 28/2014 majira ya usiku eneo la Usoke.

Umeongeza kusema kwamba siku hiyo washitakiwa walimuua askali Polisi wenye namba G3388 PC Shabani Mbua na namba G 4602 kwa kuwapiga risasi.

Askari hao wawili waliuwawa wakati wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi na usalama kwenye kituo cha Polisi Usoke wilayani Urambo mkoani Tabora mwaka 2014.

Akitoa uamuzi huo hakimu amesema mahakama imewatia hatiani kwa makosa hayo hivyo inawahukumu kunyongwa hadi kufa lakini wanaruhusiwa kukata rufaa kama hawakuridhika na adhabu hiyo.

Upande wa utetezi katika shauri hilo ulikuwa unawakilishwa na mawakili Fravian Fransisi,Amos Gaise,Chistina Jacson na Chales Hayo.

By Jamhuri