Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara
Kikosi kazi cha uwezeshaji wa mafunzo ya mwongozo wa kukabiliana na ukatili maeneo ya umma kimeifikia mikoa ya Mtwara na Lindi ambapo jumla ya washiriki 85 kutoka kwenye mikoa hiyo wamepatiwa mafunzo ya siku moja ya uundaji na uendeshaji wa madawati ya kukabiliana na ukatili maeneo ya Umma.
Mkurugenzi Msaadizi wa Maendeleo ya Jinsia, kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Rennie Gondwe, akitoa maelezo mafupi kuhusiana na mafunzo hayo amesema shabaha ni kuifikia mikoa yote 26 nchini ambapo hadi sasa tayari mikoa 10 imefikiwa.
“Leo tupo Mtwara, ambacho ni kituo cha tatu kwa awamu hii ya pili ikiwa tumeshaifikia Mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na sasa Mtwara na Lindi ambapo tumewafikia jumla ya waratibu 210 mkiwemo ninyi,” amesema Rennie.
Rennie amefafanua kuwa tayari madawati 104 yameanzishwa tangu kuasisiwa kwa Mwongozo huo mapema mwezi Februari, 2023 ulipofanyika uzinduzi mkoani Kilimanjaro.
Katika hatua nyingine Rennie amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara na mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili hivyo ujio wa Mafunzo hayo ni hatua kubwa ya kumuunga mkono, ili kusaidia wananchi kujikita kwenye shughuli za uzalishaji mali na hivyo kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Akitoa Salaam za Mkoa wa Mtwara kwa niaba ya Mikoa hiyo miwili, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa, Abdi Mfinanga amewataka washiriki hao kuzingatia mafunzo na baada ya hapo wakaanzishe na kuendesha madawati hayo.
“Ninyi ni wateule katika mafunzo haya, tunaomba mkayatendee haki, ikiwepo kuanzisha na kusimamia madawati yenye tija, hapa zimetumika rasilimali za Serikali, hivyo ili uteule wenu uwe na maana basi mkazifanyie kazi, msiende kulala na rasilimali hizi ambazo Serikali imezileta kwetu zilete matokeo chanya.” amesema Mfinanga.
Mpaka sasa kikosi kazi hicho kimeshatoa mafunzo kwa Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Tanga, na Geita. Mikoa mingine ni Morogoro, Pwani, Dar es salaam na sasa Mtwara na Lindi ambapo katika awamu hii ya pili watakamilisha na mkoa wa Ruvuma ikiwa hadi kukamilika kwake jumla ya waratibu 465 watakuwa wamefikiwa.