Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kudhibiti madhara ya mmomonyoko na kupanuka kwa kingo za mito.

Khamis amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Bagamoyo Muharami Mkengealiyetaka kujua ni lini Serikali itajenga Kingo za Mto Mpiji wilayani Bagamoyo mkoani Pwani zilizopanuka kutokana na Mvua kubwa na hivyo kuhatarisha nyumba za wananchi wa maeneo hayo.

Amesema jitihada zilizofanywa na Serikali ni pamoja na kuandaa Mwongozo wa Usafishaji wa Mito ili kuondoa mchanga na tope ambapo kikosi kazi kimeundwa kwa ajili ya kushughulikia suala la usafishaji wa mito.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali wakati wa Kikao cha Tano cha Mkutano wa 18 wa Bunge jijini Dodoma leo Januari 03, 2025.

“Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Mazingira sura 191 kifungu cha 57 (2) kimempa Waziri mamlaka ya kutunga kanuni ndogo na mwongozo na tayari kuna hatua zimeanza kuchukuliwa kwa kufanya doria na kuzuia mali au gari litakalokutwa na kupigwa faini,” amesema Mhe. Khamis.

Pamoja na hatua hiyo, Naibu Waziri Khamis ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili watambue umuhimu wa kutunza mazingira katika mito.

Aidha, ameeleza kuwa katika kudhibiti athari za mvua, Serikali inatumia njia za asili za kudhibiti mmomonyoko wa kingo za mito kwa kupanda miche 5,000 aina ya michikichi, migomba, miti maji na matete katika kingo za mto katika eneo lenye ukubwa wa ekari 100 katika Kata ya Mabwepande wilayani Kinindoni mkoani Dar e Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni akizungumza na Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba wakati wa Kikao cha Tano cha Mkutano wa 18 wa Bunge jijini Dodoma leo Januari 03, 2025. Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis.

Amesema Serikali imeweka utaratibu maalumu wa uondoaji wa mchanga kwa kuunda vikundi 12 vya Wapakia mchanga na wakandarasi 14 wa uchimbaji wa mchanga kwa utaratibu unaojulikana kama “kusafisha mto ili kuruhusu utiririshaji wa maji kwa njia ya asili”.

Mhe. Khamis amebainisha kuwa kwa mwaka 2025/26, Serikali kupitia Wizara ya Maji imepanga kutenga shilingi millioni 552kwa ajili ya ujenzi wa kingo za Mto Mpiji ambao Ujenzi utatekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/26.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa Kikao cha Tano cha Mkutano wa 18 wa Bunge jijini Dodoma leo Januari 03, 2025.